UKURASA WA 699; Mafanikio Yoyote Yanaanza Na Mtu Mmoja…

By | November 29, 2016

Watu wengi wanapoyaangalia maisha ya watu ambao tayari wamefanikiwa, huwa wanaona jinsi ambavyo wanafanya makubwa na wanagusa maisha ya watu wengi. Watu huhamasika na hilo na kuona na wao wanaweza kufika pale ambapo wengine wamefika.

Ni kweli kwamba unaweza kufika pale ambapo wengine waliofanikiwa wamefika, lakini mtazamo wa kufika pale ambao unao siyo sahihi. Watu wengi wanaofikiria kuanza huwa wanafikiria kuanza na kundi kubwa la watu.

Kama ni biashara basi anapiga mahesabu ya kuwa na wateja wengi ambao watamletea faida kubwa. Hata kama ni sanaa basi anafikiria kuanza na wafuasi au mashabiki wengi na hivyo kufanikiwa.

Lakini dunia haiendi hivyo, hakuna mafanikio ambayo yamewahi kuanza na watu wengi. Mafanikio yoyote yanaanza na mtu mmoja. Mtu mmoja ambaye anajali kile unachofanya, na kinagusa maisha yake, kisha anamwambia mwingine na mwingine na mwingine, baada ya muda, unakuta kundi la watu hawa linakua zaidi.

Huanzi biashara na maelfu ya wateja, unaanza biashara na mteja mmoja, mtu mmoja ambaye ana shida na wewe unaweza kuitatua, halafu anaendelea kukutegemea wewe kutatua shida yake, huku akiwaambia wengine kuhusu wewe na wao kuja pia.

Hata wanamuziki wakubwa unaowaona, hawakuanza na mashabiki wengi, walianza na shabiki mmoja. Wakati mwingine ndugu au mtu wa karibu aliwaambia unaimba vizuri, hebu jaribu kuingia kwenye muziki, mambo yakaenda hivyo.

Unapoyaona mafanikio yoyote rafiki yangu, hili liwe kwenye akili yako, kwamba hutaanza na watu wengi, bali utaanza na mtu mmoja, baadaye kikundi cha watu wachache, halafu unaendelea kukua.

Nakukumbusha hili rafiki ili;

  1. Ukumbuke kuwa mvumilivu kwenye safari yako ya mafanikio, usikate tamaa kwa sababu wanaoenda na wewe kwa sasa ni wachache, watumie wachache hao kuwafikia wengi zaidi.
  2. Kuwa na mtazamo sahihi wa kuanza, usikimbilie kuanzia juu kabla ya kujenga msingi chini.
  3. Kumbuka mafanikio yoyote yanahitaji muda. Kutoka mtu mmoja mpaka watu wengi kuna muda unahitajika.

Ni vizuri kuwa na picha kubwa ya mafanikio, lakini kumbuka unaanza na mtu mmoja. Chagua nani unataka kuanza naye katika mafanikio unayotengeneza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.