UKURASA WA 717; Maamuzi Ya Kukurupuka…

By | December 17, 2016

Hakuna kitu kinatuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu kama maamuzi ya kukurupuka. Unakuta mtu unafanya maamuzi bila ya kufikiri kwa kina na mwishowe yanakuwa na madhara makubwa kwako. Wakati unafanya maamuzi hayo unaona kila kitu kipo sawa, lakini unapokuja kukaa chini na kufikiri kwa kina, unaona namna ulifanya maamuzi bila ya kuwa na taarifa sahihi.

Hii pia ni njia ambayo imekuwa inatumiwa na watu wanaotaka kukulaghai au kukutapeli. Watu ambao wanataka kukusukuma ufanye kile ambacho wanataka wao, ambacho hakina manufaa yoyote kwako ila kina manufaa makubwa kwao. Wanahakikisha unakurupuka na kufanya maamuzi bila ya kuwa na taarifa sahihi. Wanahakikisha hawakupi muda w akufikiri kwa kina ili ukimbilie kufanya maamuzi ambayo yatawanufaisha wao.

Hii ni tabia ambayo unahitaji kuivunja haraka sana kama unataka kufanikiwa na kudumu kwenye mafanikio. Na jinsi ya kuivunja tabia hii ni kuzingatia yafuatayo;

Jiridhishe na taarifa kabla hujafanya maamuzi.

Kabla hujafanya maamuzi yoyote makubwa na muhimu, jiridhishe na taarifa unazopata. Je ni taarifa za kweli, je ni taarifa sahihi, je ni taarifa za kutosha. Mara nyingi watu wanaweza kuwa na taarifa ambazo siyo za kweli, au taarifa za kweli lakini hazijajitosheleza, wanazitumia kufanya maamuzi na wanaumia. Chunguza taarifa ulizonazo kwa makini, usiamini maneno ya watu tu, nenda mbali zaidi kujiridhisha na kile unachoambiwa au unachoona.

Muda ni silaha yako muhimu.

Muda ni tiba ya kila kitu, hakuna kinachoweza kuushinda muda. Siku zote kama siyo jambo la kufa na kupona, basi lipe muda. Ninaposema jambo la kufa na kupona namaanisha kitu ambacho unahitaji kuchukua hatua mara moja la sivyo unakufa au mtu anakufa. Labda nyumba inawaka moto na watu wapo ndani ya nyumba hiyo. Hapa unahitaji kuchukua hatua haraka, lakini pia bado huhitaji kukurupuka. Kwa mambo mengine, jipe muda kabla hujafikia uamuzi kamili. Kwa mfano kuna kitu umekutana nacho na unataka kukinunua, usikinunue kwanza, hata kama hela unayo. Jipe muda wa kulitafakari hilo kwa kina, na utaona kama ni muhimu kwako au la.

Epuka kuendeshwa kwa hisia.

Maamuzi mengi tunayofanya kwenye maisha yetu, yanaendeshwa na hisia. Na hisia kuu zipo mbili, furaha na hasira. Kamwe kamwe usifanye maamuzi ukiwa na furaha sana au ukiwa na hasira sana, lazima tu utakosea. Kwa sababu mara zote hisia zinazuia uwezo wetu wa kufikiri kwa kina. Hivyo unapokuwa kwenye hali ya furaha, au hali ya hasira, jizuie kabisa kufanya maamuzi yoyote, utakuja kuyajutia.

Tumia kauli ya Richard Branson.

Richard Branson ni mjasiriamali bilionea wa nchini Uingereza, ana makampuni zaidi ya 400. Kuna kauli yake moja ambayo huwa naitumia kila mara. Anasema fursa za kibiashara ni sawa na mabasi ya abiria, mara zote kuna basi jingine linakuja. Kama ambavyo unajua, daladala moja ikipita, basi ipo nyingine inakuja. Hii ni muhimu kuitumia kuepuka kukurupuka na kuvamia fursa kwa sababu tu watu wanakuambia inapita au hautaiona tena. Usisukumwe kuingia kwenye fursa ambayo huijui vizuri, fursa zipo nyingi mno.

Fanyia kazi haya ili kujijengea nidhamu ya kuwa na subira kabla ya kufanya maamuzi makubwa kwenye maisha yako. Epuka kukurupuka kwenye jambo lolote lile na pia jifunze kwenye kila unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.