Kuhusu utajiri tu, mengi yanasemwa, mengi yanaandikwa na kila mtu ana lake la kusema. Lakini kama ujuavyo, maoni ni mengi ila ukweli ni mmoja. Na kwa kuwa mara nyingi ukweli huwa unaumiza, wengi hawapendi kuusikia na hivyo kukimbilia maoni.
Utasikia watu wakikuambia lima zao fulani utakuwa tajiri, au fuga kitu fulani utakuwa tajiri. Wengine watakuambia somea kitu fulani na utakuwa tajiri, au pata utaalamu fulani na utakuwa tajiri. Wapo watakaokuambia wekeza maeneo fulani na utakuwa tajiri, nunua hisa za kampuni fulani na utajiri utakuwa wako. Utasikia pia kuhusu utajiri unaopatikana kwa kufanya biashara kupitia mtandao wa intaneti.
Zote hizi zinazotajwa na njia za kukupeleka kwenye utajiri, kama ni safari basi hayo ni mabasi. Kama ambavyo ukitaka kutoka Dar kwenda arusha, unaweza kupanda basi la Kilimanjaro, Dar Express, Machame, Ngorika na mengine mengi. Hivi unavyoambiwa siyo vyanzo vya utajiri, bali njia za kukufikisha kwenye utajiri, ambapo yoyote itakufikisha iwapo tu utakuwa na kile chanzo halisi cha utajiri ndani yako.
Na chanzo kikuu cha utajiri ambacho kipo ndani yako ni tabia zako. Hivyo tu, yaani tabia zako ndizo zitakuletea utajiri au kukuzuia kufikia utajiri. Hakuna zaidi ya hapo, siyo elimu, siyo rangi na siyo umri, bali tabia zako.
Kama tabia zako haziendani na maisha ya utajiri, hata ungepewa fedha kiasi gani bado utatafuta njia ya kurudi kwenye umasikini. Kama ambavyo wale wanaoshinda mamilioni kwenye michezo ya bahati nasibu wanavyokuwa masikini baada ya muda mfupi.
Na kama tabia zako zinaendana na maisha ya utajiri, utapata utajiri bila ya kujali ni njia ipi umechagua kupita, ila tu iwe njia halali.
Tabia zipi zinaendana na maisha ya utajiri? Kuwa na maono makubwa, kujituma, kuweka akiba, kuwa na nidhamu ya fedha, kuwekeza na kuwa bora zaidi kila siku. Hizi ni baadhi tu ya tabia za utajiri.
Tabia za umasikini ni kama kukosa maono makubwa, uvivu, kulalamika, kusubiri vya kupewa, kukosa nidhamu ya fedha, kuwa na madeni kila mara na kutaka kuwarudisha nyuma wengine.
Kama ambavyo nimewahi kukuambia, uzuri wa tabia ni kwamba, unachagua wewe mwenyewe. Hakuna mtu anakulazimisha uwe na tabia fulani, ni wewe mwenyewe unachagua tabia ulizonazo. Hivyo basi, chagua tabia za utajiri na njia yoyote utakayopita itakufikisha kwenye utajiri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK