UKURASA WA 733; Wakati Sahihi Wa Kufanya Mabadiliko Ni Huu…

By | January 2, 2017

Pale mambo yanapokwenda vizuri, sisi binadamu tuna tabia ya kujisahau, tunaanza kuona mambo yanakwenda vizuri kwa sababu labda sisi ni wajanja sana, au labda tuna bahati sana, au sisi ni zaidi ya wale ambao mambo yao hayaendi vizuri.

Tunapojisahau hivi kwa muda mrefu, tunakuja kustuka mambo yakiwa hayaendi vizuri kama awali. Tunastuka matokeo ni tofauti na tulivyotegemea, tofauti na tulivyozoea.

Nini kinatokea kwenye wakati huu? Tunataharuki na kuanza kufanya mabadiliko makubwa na ya haraka ili kunusuru hali isiendelee kuwa mbaya zaidi.

Lakini nini ambacho huwa kinatokea? Tunazidi kuharibu zaidi, tunazidi kufanya mambo kuwa mabaya zaidi. Tunafanya kwa lengo la kunusuru, lakini tunajikuta tukiharibu zaidi.

Ili tusifike kwenye hali kama hii, tunahitaji kuanza kuchukua hatua mapema, tunahitaji kuanza kufanya mabadiliko mapema. Je mapema ni ipi? Ni wakati upi sahihi wa kufanya mabadiliko ili mambo yasiende vibaya?

Jibu ni wakati ambapo mambo yanakwenda vizuri ndiyo wakati wa kufanya mabadiliko. Hufanyi mabadiliko ili kuharibu yale yanayoenda vizuri, bali unafanya mabadiliko ili kuhakikisha unabaki na matokeo yale mazuri.

Wakati mambo yanakwenda vizuri, unakuwa na uhuru mkubwa wa kujaribu njia mpya, wa kuangalia fursa tofauti ambazo unaweza kuzitumia kuendelea kupata matokeo mazuri. Kwa kufanya hivi unakuwa mbele zaidi na hivyo mabadiliko yoyote yanapotokea, na lazima yatokee yanakukuta wewe uko upande mzuri.

Usijisahau pale mambo yanapokwenda vizuri, huu ndiyo wakati wa kujaribu mambo mengi ili kupata njia bora zaidi za kuhakikisha unapata matokeo bora zaidi. Ukisubiri mpaka unapokuwa kwenye changamoto, utakuwa na hofu ya kujaribu mambo mapya na kila hatua ya kujinasua unayochukua inakudidimiza zaidi.

Chukua hatua za mabadiliko sasa, wakati mambo yapo vizuri. Utakuwa kwenye nafasi nzuri pale mambo yatakapobadilika, na lazima yabadilike.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.