UKURASA WA 743; Utengano Ni Muhimu Kwa Mafanikio Yako…

By | January 12, 2017

Kutoka hapo ulipo sasa na kufika kwenye ndoto ya maisha yako, kuna vitu unahitaji kutengana navyo. Yaani kuna vitu ambavyo lazima uviache ili uweze kufika kule unakotaka kufika. Hili ni somo muhimu ambalo watu wengi wamekuwa hawalielewi.

Ndiyo maana mabadiliko yanakuwa magumu sana kwa watu wengi. Kwa sababu wanachotaka wao ni kufikia mafanikio makubwa, lakini waendelee na maisha waliyonayo sasa. Kitu ambacho siyo tu hakiwezekani, bali pia ni kichekesho. Ni kichekesho kwa sababu kufikiria kwamba unaweza kufikia mafanikio kwa kuendelea na mambo yale yale unayofanya kila siku, ni kujidanganya, kwa sababu haiwezekani kwa namna yoyote ile.

SOMA; Mafanikio Ya Wengine Ndiyo Mafanikio Yako…

Najua unajua hili, lakini leo nataka tuliangalia kwa upande wa pili.

Wakati unapoweka mipango na mikakati yako ya mafanikio, usiishie tu kuangalia yale unayoyapata na hatua za kuchukua, bali pia jiulize, je nakwenda kutengana na nini? Ni vitu gani ambavyo utakwenda kuacha kufanya ili uweze kufikia ndoto zako? Ni muhimu kujua haraka ili kuweza kujiandaa na isiwe jambo la kushangaza kwako.

Baadhi ya vitu utakavyokwenda kutengana navyo vitakuumiza sana kwa sababu ulishavichukulia kama sehemu ya maisha yako. Lakini hakuna namna, ili uweze kupiga hatua zaidi ni lazima uweze kuacha kile unachokipenda na ulichokizoea sasa na kuendea kitu kipya ambacho wakati mwingine huna uhakika kama kitafanya kazi.

Kuna watu pia ambao utahitaji kutengana nao ili uweze kupiga hatua za kukufikisha kule unakotaka kufika. Watu hawa wanaweza kuwa wa karibu sana na mmekuwa pamoja kwa muda mrefu, ila kwa ndoto kubwa uliyonayo sasa, wanaweza kuwa kikwazo badala ya kuwa hamasa. Ukishaliona hilo inabidi ukubali utengano huu ili uweze kupiga hatua.

Chagua kuchukua hatua kwa kuwa tayari kutengana na vitu ambavyo kwa sasa umeshavizoea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.