UKURASA WA 746; Jiwekee Ukomo Wa Muda…

By | January 15, 2017

Sheria ya Parkinson inasema, kazi yoyote inachukua muda ambao imetengewa kufanyika. Kwa mfano kama umetenga masaa mawili kwa ajili ya kufanya kazi fulani, utatumia masaa hayo mawili kuifanya. Na kazi hiyo hiyo kama una nusu saa ya kuifanya, utatumia nusu saa hiyo kuifanya na kuikamilisha.

Jukumu lolote unalofanya, ukamilishaji wake unategemea muda ambao unao wa kukamilisha. Kama muda ni mwingi sana unajikuta ukipoteza muda mwingi katikati lakini mwishoni utaweka juhudi na kuweza kumaliza kwa wakati. Kama muda ni mdogo wa kufanya kitu, utajikuta unatunza sana muda huo na kuhakikisha unautumia kwenye kazi hiyo tu.

Sasa tunahitaji kuitumia sheria hii vizuri, kwetu sisi wenyewe ili tuweze kutumia vizuri muda wetu na kufanya makubwa.

Kwa kawaida huwa tunapanga kuanza kufanya kitu, ila huwa hatupangi tutamaliza kufanya saa ngapi. Tunajipa muda wote tulionao kufanya kitu hicho. Kwa njia hii mambo mawili hutokea;

SOMA; Kubishana Ni Kupoteza Muda Wako…

Jambo la kwanza tunatumia muda vibaya, kwa sababu tunaona upo tu wa kutosha, hivyo tunafanya bila ya haraka yoyote.

Jambo la pili tunakosa hamasa na kuchoka haraka, kwa kuona tuna muda mwingi zaidi wa kufanya kitu hicho, tunachoka.

Ili kuondokana na hayo na kuweza kutumia muda vizuri, jipe ukomo wa muda kwa chochote kile ambacho unakifanya. Na ukomo huu uwe mdogo, yaani usijiwekee muda mwingi halafu ukaupoteza.

Kwa mfano jipe saa moja ya kutekeleza kazi yako bila ya kufanya kitu kingine. Kama unaingia kwenye mitandao ya kijamii, jipe dakika tano tu. Kila unachofanya, jipe ukomo wa muda, kwa njia hii utaiona thamani ya muda wako ni kuweza kuutumia vizuri.

Usikubali muda uende wenyewe unavyotaka, bali dhibiti matumizi ya muda wako, kwa kuhakikisha unakuwa na ukomo kwenye kila jukumu ulilopanga kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.