UKURASA WA 767; Dhibiti Dunia Yako…

By | February 5, 2017

Dunia ipo hivi,

Unaweza kuchagua kudhibiti kila ambacho kipo chini yako na kuyapeleka maisha yako namna unavyotaka.

Au wengine wanaweza kudhibiti kila kilicho chini yako, pamoja na kukudhibiti wewe pia na kujikuta unaishi maisha ambayo huyaelewi. Unaona upo tu, unasukuma siku lakini hupati kile ambacho unataka.

Anza na kujidhibiti wewe mwenyewe, jijengee nidhamu ya kufanya kile ambacho umepanga kufanya kwa wakati uliopanga kufanya. Ukishindwa kujidhibiti wewe mwenyewe, utatumbukia kwenye mikono ya wengine ambao watakudhibiti watakavyo, watakufundisha nidhamu ya kuwanufaisha wao.

Dhibiti sana mawazo na fikra zako, akili yako ndiyo hazina yako, ndiyo inayokuletea kila ulichonacho sasa. Unahitaji kuidhibiti kwa kuchagua ni taarifa gani unazoruhusu ziingie. Ukiruhusu mawazo hasi na ya kukata tamaa yaingie, hutaweza kupiga hatua. Ukishindwa kudhibiti kinachoingia kwenye mawazo yako, wengine watadhibiti watakavyo, watakulisha kila aina ya habari kuhakikisha wanatimiza madhumuni yao.

SOMA; Siyo Kwamba Dunia Haina Huruma, Dunia Haina Muda Na Wewe.

Dhibiti sana muda wako, kila sekunde na dakika yako hakikisha unaitumia kufanya jambo ambalo ni muhimu kwako katika kufikia ndoto zako. Ukishindwa kudhibiti muda wako, wengine watautumia wanavyotaka wao kutimiza madhumuni yao.

Dhibiti kazi unayoifanya, usifanye kitu hivyo hovyo, fanya kitu kwa viwango vya juu sana. Fanya kitu cha tofauti, kitu ambacho wengine wakikiona wanahamasika kufanya kazi na wewe. Wanatamani ufanye kazi kama hiyo kwa ajili yao pia.

Dunia ni namna unavyoidhibiti, vile unavyoidhibiti ndivyo inavyokupa kile unachotaka, ukishindwa kuidhibiti utaishia kukubali kila kinachokufikia.

 

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.