Kwenye maisha wapo watu ambao wanatenda, watu ambao wanachukua hatua, kuendea ndoto zao kubwa ambazo wanazo kwenye maisha yao. Watu hawa wanajua nini wanafanya na kwa wakati gani. Wanajua hatua zipi wanahitaji kuchukua kila siku ili kuweza kufikia ndoto zao. Hawa ni watu wachache, na ndiyo wanaofikia mafanikio makubwa, kwa sababu kila wanachofanya kimepangiliwa na wanajua kwa nini wanafanya.
Kwa upande wa pili, lipo kundi kubwa, la watu ambao hawawezi kutenda, badala yake wanaitikia matendo ya wengine. Wao hawawezi kuchukua hatua, ila watasubiri mpaka wengine wachukue hatua, halafu wanaitikia. Wanaweza kuitikia kwa kukosoa, kukatisha tamaa au hata kuiga. Kwa vyovyote vile, ni kitu ambacho hata hawakuwa wanakijua kabla, lakini wanakutana nacho na ghafla wanaitikia.
Hivi ndivyo wanavyofanya wengi ambao wanashindwa kufanikiwa, wengi ambao wanakuwa na maisha ya kawaida, huku wakiwashangaa wale wanaopiga hatua kwenye maisha yao. Hawa wataamka siku yao na kuanza kusikiliza habari, nini kimetokea halafu wanaanza kuchangia kama vile walijipanga kwa kitu hicho. Watu hawa wana maoni kwenye kila jambo linalotokea au analofanya mtu. Lakini hawajui nini wanafanya siku inayofuata, pia hawajioni wako wapi miaka kumi ijayo.
SOMA; Sababu Ya Wewe Kutenda Wema…
Ninachotaka kukuambia rafiki yangu, na lengo la kukuandikia hapa leo ni hili; kuwa mtendaji, kuwa mchukuaji wa hatua na usiwe mwitikiaji wa wanayofanya wengine. Nakuambia hivi kwa sababu changamoto kubwa ya ulimwengu tunaoishi sasa ni kulazimika kuwa mwitikiaji wa mambo ya wengine, maana tumeunganishwa na dunia nzima, na tuna nafasi ya kujua kila kinachoendelea kwenye maisha ya mtu.
Tunajua mtu kavaa nini leo, laka nini mchana na hata amegombana lini na mwenzi wake. Sasa hivi sivyo tunavyopaswa kwenda kama mafanikio ndiyo tunachotaka.
Wazungu wanasema MIND YOUR OWN BUSINESS, ikiwa na maana kwamba JALI MAMBO YAKO MWENYEWE, ni vigumu kujali mambo yako kwenye dunia hii ambayo ukiingia kwenye mtandao tu unakutana na kila kitu kuhusu maisha ya kila mtu.
Hivyo lazima ufanye hivi kwa makusudi kabisa, uepuke kuitikia yale wengine wanafanya, ufanye yale ambayo ni muhimu kwako kwanza. Kwa sababu hakuna anayejali mambo yako zaidi ya wewe mwenyewe. Na muda unaotumia kufuatilia ya wengine, ndiyo muda unaopoteza kufikia ndoto zako.
Kipaumbele cha kwanza kabisa kwenye maisha yako ni ndoto zako, ya wengine yanapaswa kusubiri kwa wakati wake. Haya ndiyo maisha ya mafanikio, tunayopaswa kuyaishi kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK
Pingback: UKURASA WA 789; Kutenda Na Kuitikia Matendo Ya Wengine… — Kisima Cha Maarifa – bryanorganization
Pingback: UKURASA WA 1009; Matokeo Ni Muhimu Zaidi Kuliko Maelezo… – Kisima Cha Maarifa