UKURASA WA 804; Kama Kila Kitu Ni Kipaumbele, Huna Kipaumbele….

By | March 14, 2017

Zama tunazoishi sasa, ni zama zenye changamoto kuliko zama nyingine zozote. Kwa sababu kitu chochote unachojifunza leo, kesho kinaweza kisiwe sahihi tena. Kitu kinachokuingizia kipato leo, siku zijazo kinaweza kisiwe njia ya kuingiza kipato.

IMG-20170228-WA0004

Angalia tu namna ambavyo mbinu za uzalishaji, ufanisi, usimamizi na nyingine nyingi zinavyopitwa na wakati kutokana na ukuaji wa teknolojia na ujio wa mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Angalia namna ambavyo kazi nyingi zinakufa na kupotea kabisa, nyingine zinakosa maana, wakati siku za nyuma zilikuwa kazi za heshima.

Wapo wanaofikiri mambo yataendelea kubaki kama yalivyo, kwamba wakishapata mgodi wao, kazi kwao ni kuchimba tu. Hawa wanajidanganya na siku wataamka hawataamini kinachoendelea, maana watakuwa wameondolewa kabisa pale walipokuwa wanategemea.

Sasa, kwa ukuaji huu wa maendeleo, vitu vya kufanya vinakuwa vingi kwetu. Taarifa ni nyingi, maarifa ni mengi na watu wanaohitaji muda wetu ni wengi. Lakini masaa yetu kwa siku ni yale yale, masaa 24 tu ndiyo tunayo, hatuna zaidi ya hapo.

Hivyo njia pekee ya kuweza kufika kule tunakotaka kufika, tukiwa vizuri ni kuweka vipaumbele, katika mengi tuliyonayo ya kufanya, tunapaswa kuchagua yale machache muhimu sana, na kuachana na hayo mengine ambayo siyo muhimu.

SOMA; Uhusiano Kati Ya Mafanikio Makubwa na Kuweka Kipaumbele.

Hapa kwenye kipaumbele ndipo changamoto ilipo, kwa sababu unahitaji ufanye machache na mengine mengi uweke kando, wengi wanaumia, na kuona hawawezi kuweka kando jambo lolote. Wanaona ni lazima wao wafanye au ni muhimu kwao kufanya. Hivyo wanajidanganya kwamba kila kitu ni kipaumbele kwao. Hapo ndiyo wanadhihirisha kwamba, hawana kipaumbele chochote.

Kama unaona lazima ufanye kila kitu, kama unaona wewe tu ndiyo wa kufanya, kama kila kitu ni kipaumbele kwako, basi jua huna kipaumbele. Hujui kipi hasa unataka, na utajikuta unazunguka na mambo mengi huku matokeo yako yakiwa ni madogo mno.

Lazima ujijengee nidhamu ya kuweza kusema HAPANA, HIKI SIFANYI hata kama kinakupa raha kufanya. Kama hakina mchango mkubwa wa kule unakotaka kufika, achana nacho, litakuwa ni jambo bora sana kwako kufanya kwenye maisha.

Wanasema mshika mawili moja humponyoka, na pia wanasema mtaka yote kwa puka hukosa yote. Ya pili ni sahihi kabisa, kama unataka kufanya kila kitu, utashindwa kufanya chochote na hivyo kushindwa kupata unachotaka.

Weka vipaumbele bila ya huruma, ongozwa na kile ambacho ni bora kwako, na siyo unachofurahia kufanya. Unachohitaji ni majibu ya muda mrefu, siyo furaha ya muda mfupi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.