Kuwa na biashara pekee haitoshi, ni lazima uweze kumfikia mteja wako, na yule ambaye anafaa kuwa mteja wako ajue juu ya uwepo wako. Huu ndiyo umuhimu wa masoko kwenye biashara.
Lakini linapokuja swala la masoko, wengi wanafikiria kitu kimoja pekee, kutangaza. Na wanakazana kupata maeneo mazuri ya kutangaza, ambapo tangazo litaonekana na wengi, ambapo hiyo inapelekea gharama za kutangaza kuwa kubwa. Kwa mfano kutangaza biashara kupitia tv, hasa wakati wa taarifa ya habari, gharama zake ni kubwa zaidi.
Lakini vipo vitu vingi vya kufanya kama mfanyabiashara katika masoko licha tu ya kutangaza. Na hapa nakushirikisha viwili muhimu sana kuzingatia ili kuweza kukuza biashara yako.
Cha kwanza; mjali sana mteja wako.
Utakuwa unajisumbua na kupoteza fedha na muda, iwapo utakazana kutangaza biashara, halafu mteja akifika kwenye biashara yako hajaliwi. Hapati kile anachotaka na wala hakuna anajali kuhusu uwepo wake.
SOMA; Sababu Moja Ya Kukufanya Uingie Au Uendelee Kubaki Kwenye Biashara Yako…
Hakuna njia rahisi ya kutangaza biashara yako kama kupitia wateja wako. Pale wateja wanaporidhika, wanakuwa tayari kuwaambia wengine kuhusu biashara yako na wale wanaoambiwa wanakuja kujaribu pia. Wakipata huduma bora, wakijaliwa, wakiheshimiwa, watakuja tena na tena na kuwakaribisha wengine.
Hivyo kwenye biashara yoyote, kumjali mteja ni hatua muhimu sana. Kama hujali kuhusu wateja wako, unafanya biashara ili nini? Maana muda siyo mrefu hutakuwa na wateja tena, hata kama unatangaza kiasi gani.
Cha pili; kupima.
Kama mfanyabiashara laima upime, pima kila kitu kwenye biashara yako, hasa kwenye masoko. Usipopima huwezi kuelewa kama unachofanya ni sahihi au la. Pia huwezi kujua wapi unakosea ili kurekebisha. Kwa kila kitu unachofanya kwenye biashara yako, pima kinaleta matokeo gani kwenye biashara hiyo. Kinaongeza wateja zaidi? Kinaongeza mauzo zaidi? Vipi kuhusu faida? Vipi kuhusu wateja kurudi tena na tena?
Lazima uwe na namba zinazokuonesha hatua uliyochukua imekuwa na mchango gani kwenye biashara yako. Na namba ndiyo zinakuonesha wazi kipi kinachotokea.
Wajali wateja na pima kila unachofanya kwenye biashara yako. Haya yatakuwezesha kukuza biashara yako na kuwafikia watu wengi zaidi, bila hata ya kutumia gharama kubwa kutangaza.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK