Nini kinakuamsha asubuhi na mapema ili uwahi kwenye kazi au biashara yako? Au kipi kinakufanya uchelewe kurudi nyumbani au uchelewe kulala kwa kuwa kwenye kazi au biashara yako? Hili ni swali muhimu sana ambalo kwa kuliangalia kwa undani utaona nani anaweza kufanya makubwa na hata kufanikiwa.
Ipo misukumo mbalimbali inayowafanya watu kufanya kile wanachofanya.
Wapo watu ambao wanafanya kile wanachofanya, kwa sababu kuna kitu wanakitaka kwa wakati huo. Hivyo wanajua wakifanya watapata wanachotaka, na hivyo kusukumwa kufanya. Sasa kwa kuwa kuna wanachotaka, wakishakipata msukumo wa kufanya nao unapungua. Hivyo anakuwa hana hamasa tena kama mwanzo. Angalia watu ambao walikuwa wanatafuta kazi kwa sababu tu wanataka waonekane nao wana kazi, hakuna kazi kubwa wanayofanya, maana kilichokuwa kinawasukuma kimetimia. Kadhalika wale wanaoingia kwenye kazi au biashara kwa sababu wanataka fedha, wakishazipata fedha, ufanisi unapungua.
Wapo watu ambao wanafanya kile wanachofanya wakiwa hawahitaji chochote sasa hivi, lakini wanajua baadaye watahitaji kitu na wanachofanya sasa kitawasaidia. Hawa wanaangalia mbele zaidi, wanaweza kuwa hawahitaji sasa, lakini wanajua siku zijazo watahitaji, na hivyo kujitoa kufanya sasa. Hawa ndiyo wale ambao wanaweka juhudi kubwa kwenye kazi hata kama hawalipi kiasi kikubwa. Au wale wanaoanzisha biashara zao wakiwa hawana uhitaji wa fedha kwa wakati huo, lakini wanajua baadaye watahitaji na biashara hizo zitawasaidia.
SOMA; Vitu Viwili Muhimu Vya Kufanya Kwenye Masoko….
Kundi la tatu ni wale ambao wanafanya kitu kwa sababu wanataka kufanya, hakuna chochote wanachotaka, wala hawategemei kupata ila wanafanya kwa sababu wana weza kufanya na wapo tayari kufanya. Hawa ni wale ambao wameshafikia kiwango cha juu cha kujitambua, ambao wameshaweza kutenganisha kufanya na kupata, na wao wanafanya ili kutoa mchango wao kwa wengine, siyo kwa sababu wanategemea kupata matokeo fulani.
Katika makundi haya matatu, kundi la kwanza hufa masikini, kwa sababu hawawezi kufanya makubwa kama hawana uhitaji, na mara zote uhitaji wa haraka siyo unaoleta mafanikio. Kundi la pili wanakuwa matajiri lakini wanaweza wasiwe na amani ya moyo kwa sababu kuna mchango muhimu ambao hawakuweza kutoa. Na kundi la tatu, hawa wanakuwa matajiri na wanakuwa na amani ya moyo kwa sababu upo mchango mkubwa ambao wanatoa kwa wengine.
Kama ilivyo kwenye mambo mengine, hapa pia ni uchaguzi wako binafsi, unataka kuwa kwenye kundi lipi? Huo ni uchaguzi wako binafsi na popote ulipo sasa kama ni chini, unaweza kwenda juu zaidi.
Maisha ni yako na uchaguzi ni wako, chagua sasa ili uwe na maisha bora.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK