UKURASA WA 882; Wewe Ni Kazi Ya Sanaa…

By | May 31, 2017

Kwenye ukurasa wa 881 jana nilikuambia kitu kimoja, kwamba kabla hujawa bora kwenye jambo lolote unalofikiria, iwe ni kazi, biashara au uongozi, unahitaji kuwa bora wewe kwanza.

Leo nakwenda kukupa sehemu nyingine muhimu ya hilo la kuwa bora wewe kwanza, ambalo ni wewe ni kazi ya sanaa. Kabla sijaendelea kwanza nikupe sifa moja ya kazi ya sanaa; huwa haikamiliki.

Hakuna kazi ya sanaa inayokamilika. Mwulize msanii yeyote, mwimbaji yeyote, mwandishi au hata mchoraji, kwenye kazi yake yoyote aliyofanya, atakuambia yapo maeneo ya kuboresha zaidi. Kazi yoyote ya sanaa ina nafasi ya kuboreshwa zaidi. Na wasanii wanaojua hili huwa wanafanikiwa kwa sababu hawaridhiki na popote walipofika.

Nikija kwako wewe, kwa dhana ya kuwa bora wewe mwenyewe, ni kazi ya sanaa. Kwa maana kwamba haikamiliki, haina mwisho. Hakuna siku utaamka na kusema leo nimeshakuwa bora kabisa, sina tena cha kuboresha, sina tena cha kujifunza. Ukifikia hali hiyo kuna kitu kimoja cha uhakika naweza kukuambia, kwamba unaanza kuporomoka.

Katika kujiboresha wewe mwenyewe ni zoezi endelevu. Hutafika wakati useme umeshaweza kila kitu, hutafika mahali useme umeshajua kila kitu, na mara nyingi napenda kuwaambia watu, maisha ya kuwa bora ni shule ambayo haina kuhitimu.

Kila siku unayo nafasi ya kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa jana yake. Kila unachofanya unaweza kukifanya kwa ubora zaidi ya ulivyofanya wakati uliopita. Na hii ndiyo njia pekee ya kupona kwenye ulimwengu wa sasa, ambapo mabadiliko yanatokea kwa kasi ya ajabu sana.

SOMA; Kazi Itakayojimaliza Yenyewe…

Hivyo, hakikisha unaweka juhudi kwenye kujiboresha wewe kwanza, na jua hili ni zoezi endelevu, halina mwisho kama bado upo hai. Ni kama ilivyo kazi ya sanaa, ambayo mara zote inaweza kufanywa kuwa bora zaidi. Ndivyo ulivyo wewe pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.