Moja ya kitu kinachowarudisha watu wengi nyuma ni chuki. Chuki kwa watu au vitu ni jambo linalowarudisha wengi nyuma kwa sababu ukikichukia kitu unakuwa umefungwa nacho.
Kwa mfano tuseme unamchukia mtu fulani ambaye alikufanyia mambo mabaya, hii ina maana kwamba, ili chuki yako ifanye kazi, lazima kila wakati uwe unamkumbuka mtu huyo na yale mabaya aliyofanya. Yaani kila unapomuona, inabidi ujikumbushe ubaya wake. Kila unaposikia akitajwa, inabidi ujikumbushe ubaya wake ili chuki yako iendelee.
Kadhalika kwenye vitu, chochote unachochukia, inabidi kila mara ujikumbushe kwa nini nakichukia.
Unaona sasa namna gani chuki ni kifungo. Haikuruhusu hata kidogo usahau jambo lolote na kusonga mbele, kwa sababu ukisahau chuki itaondoka, inabidi uendelee kujikumbusha ili ile chuki iendelee kuwepo.
Hii ndiyo sababu chuki haijawahi kuwa na manufaa kwa mtu yeyote yule, hivyo sitegemei wewe rafiki yangu uwe na chuku kwa mtu au kitu chochote kile. Kwa sababu kitendo tu cha kuwa na chuki, maana yake umefungamana na mtu au kitu kile, hutaki kukiachia kabisa.
SOMA; Kulalamikia Nguvu Ya Mvutano….
Sasa kama ni mtu amekufanyia ubaya, au kitu ambacho kimekuangusha, unataka kweli kuendelea kufungamana nacho maisha yako yote? Naamini jibu lako ni hapana, hutaki kuendelea kufungamana na chochote ambacho kimekurudisha nyuma. Kwa sababu kufungamana huko kunakufanya uendelee kuwa nyuma.
Unachotaka wewe ni kusonga mbele, licha ya kukutana na changamoto na vikazo, unahitaji kusonga mbele, kuweka juhudi kubwa, kuwa na mtazamo sahihi ili kuweza kupata matokeo bora.
Hili halitatokea kama utakuwa na chuki ya aina yoyote ile. Hata kama ni haki yako kabisa kuwa na chuki, unaweza kuchukia mtu au kitu utakavyo, lakini ninachokuambia ni kwamba chuki hiyo haitakuwa na msaada wowote kwako, kabisa.
Hivyo jambo jema na la muhimu kwako unaloweza kufanya ni kusamehe. Unaposamehe kila mtu, wewe unayesamehe ndiye unayenufaika kuliko hata yule ambaye unamsamehe. Unaposamehe unatangaza uhuru kwako binafsi, unavunja vifungo vyako na yule ambaye amekufanyia mabaya. Unakuwa huru kuweza kufanya mambo mengine, na kuachana na yale ambayo yamekurudisha nyuma.
Unaposamehe unaruhusu akili yako kuziona fursa bora zaidi, unaondoka kwenye mtazamo ulionao wa kulaumu na kuona wewe ni wa kuonewa na kwenda kwenye mtazamo wa wewe kushika hatamu ya maisha yako.
Unaposamehe unajipa ruhusa ya kuchukua hatua, huhitaji kujikumbusha kila mara kwamba nani ni mbaya au nani unapaswa kumchukia maisha yako yote. Unakuwa huru na maisha yako, na kuweza kufanya makubwa zaidi.
Kusamehe haimaanishi kukubali watu kuendelea kukuumiza na kutumia vile watakavyo wao. Kama mtu ameshafanya jambo ambalo limekurudisha wewe nyuma, na unaona kabisa kwamba hilo ndiyo lilikuwa kusudi lake, msamehe kisha achana naye. Usimpe tena nafasi ya kufanya lile ambalo amefanya.
Kwa njia hii unakuwa hujafungwa naye, kwa sababu huna chuki, na pia humpi tena nafasi ya yeye kufanya kile ambacho amedhamiria kufanya ili kukurudisha wewe nyuma.
Una maisha haya uliyonayo sasa pekee hapa duniani, haina maana kuyapoteza kwa kujifunga na watu waliokukosea, waliokuangusha na hata kukutesa. Una dunia kubwa ya kuishi, una mengi ya kufanya na una maono makubwa ya kufanyia kazi. Hebu peleka nguvu zako huko na achilia wote ambao umewashikilia mpaka sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Asante