UKURASA WA 972; Pamoja Na Changamoto Zao, Maisha Yetu Hayana Maana Bila Ya Watu…

By | August 29, 2017

Changamoto zote tunazokutana nazo kwenye maisha yetu, zinahusisha watu wengine. Iwe umedhulumiwa ni mtu kafanya hivyo, umeumizwa mara nyingi ni mtu kafanya hivyo.

Kuna wakati tunaweza kufikiria kama watu hao wanaofanya maisha yetu kuwa na changamoto wasingekuwepo basi maisha yetu yangekuwa rahisi na mazuri sana.

Na hapo ndipo tunapokosea. Maisha hayawi rahisi kwa kuondoka kwa wale watu ambao tunaona wanayafanya maisha yetu kuwa magumu. Bali watu hao ndiyo wanayafanya maisha yetu kuwa na maana.

Hebu fikiria iwapo ungekuwa peke yako kwenye hii dunia, maisha yangeendaje? Ungekazana kufanya nini na kwa ajili ya nani?

Kwa sababu chochote unachofanya kwenye maisha yako, kusudi kubwa ni kwa wengine. Watu ni madaktari ili kuwatibu wengine wanaoumwa, walimu kuwafundisha wengine. Na unapofanya biashara, ipo wazi kabisa kwamba hufanyi biashara kujiuzia wewe mwenyewe, bali utawauzia wengine chochote unachouza.

Hivyo watu wengine ni muhimu sana kwetu, ndiyo wanaokamilisha maana ya maisha yetu.

Lakini watu hawa wana changamoto zao pia, wana mapungufu yao. Njia bora ya kuweza kwenda nao, ni kuwakubali vile ambavyo walivyo, na kusonga mbele.

Usikazane sana kutaka kumbadili kila mtu au kumnyoosha kila mtu. Badala yake chagua wale ambao unaweza kuvumilia changamoto na mapungufu yao, kutokana na manufaa wanayokuja nayo pia, kisha wakubali kama walivyo.

Dunia ina watu zaidi ya bilioni saba, hutakutana nao wote na hivyo usione kama kuwakubali watu ni mzigo mkubwa kwako. Badala yake unachagua wale ambao unaweza kwenda nao.

Kwa mfano, katika mahusiano yako, chagua kuwa na watu ambao wana mchango kwako na unaweza kuwakubali vile walivyo, pamoja na mapungufu au changamoto. Usichague watu ambao wanakuja na mzigo pekee bila ya manufaa yoyote kwako. Na usichague watu ukijidanganya kwamba utawabadili, unatafuta matatizo zaidi.

Katika kazi pia, chagua kufanya kazi na watu ambao wana kitu wanachangia kwako. Chagua kuwa katikati ya timu ambayo inakufanya uweke juhudi zaidi, uweze kupiga hatua zaidi. Halafu hizo changamoto zao nyingine zichukulie kama zilivyo.

SOMA; UKURASA WA 738; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…

Kwenye biashara hili ndiyo muhimu kabisa, wateja wanakuja na changamoto zao. Hivyo chagua aina ya wateja ambao biashara yako itawahudumia, utawakubali wateja wale jinsi walivyo na kukazana kuwapa huduma bora kabisa. Kama wapo wateja wanaokufanya uone biashara yako kama shimo la moto, achana nao tu, wapo wengine wengi unaoweza kuwahudumia vizuri.

Pamoja na kuwakubali watu, bado unapaswa kujiwekea viwango ambavyo utavitaka kwa wale ambao utawakubali vile walivyo. Hivi ni vitu ambavyo watu wanapaswa kuwa navyo, ili uweze kushirikiana nao kwenye jambo ambalo unahitaji kushirikiana nao.

Unaweza kuwa na vigezo vyako namna unavyopenda na kulingana na kile unachofanya, lakini vitu kama uaminifu, uadilifu, uchapa kazi visikosekane kwa wale watu ambao unataka kushirikiana nao.

Kuna vitu vikikosekana, hata kama kuna manufaa mengine, yanaweza kuwa mwiba zaidi. Kwa mfano kujihusisha na mtu ambaye siyo mwaminifu, hata kama anachapa kazi kiasi gani, uchapa kazi wake unaweza kuwa maumivu zaidi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.