Nimewahi kukuandikia siku za nyuma kwamba wapo watu ambao wanaishi na sisi hata baada ya kufa. Hawa ni watu ambao tunawakumbuka na kutumia mifano yao kwenye maisha yetu ya kila siku. Licha ya wao kuondoka hapa duniani, lakini ipo alama waliiacha ambayo tunaitumia mpaka sasa.
Yawezekana watu hawa ni watu wakubwa na maarufu, au watu wa karibu kwetu ambao walikuwa na mchango mzuri kwetu.
Ukienda kwenye shughuli yoyote ya msiba, ambapo mtu aliyefariki anaagwa kwa mara ya mwisho, huwa kuna utaratibu wa kusomewa historia ya marehemu. Katika historia ya marehemu, huwa tunasikia vile vitu ambavyo marehemu alifanya, hasa vile vizuri, jinsi alivyoishi maisha yake.
Huwa hatusikii kuhusu nini anamiliki wala nani alikuwa anashindana naye. Hatusikii wapi alikwama au nani alikuwa anamchukia.
Hili linatufanya tujifunze kitu muhimu sana kuhusu maisha yetu, hasa baada ya sisi kuondoka hapa duniani. Kwa sababu tutaondoka, hilo halina ubishi, kila mtu aliyewahi kuishi hapa duniani miaka 200 iliyopita alikufa.
Napenda leo tujikumbushe vitu viwili muhimu ambavyo utakwenda navyo kaburini. Ninaposema unaenda navyo kaburini simaanishi vinakufa pale wewe unapokufa, bali hata baada ya kufa, vitaendelea kuishi.
Kitu cha kwanza ni jina lako zuri ulilojijengea kwenye maisha yako. Kwa kile ambacho ulikuwa unafanya, iwe ni biashara, kazi, uongozi na kadhalika. Jina lako kama lilikuwa zuri, yaani ile sifa ambayo ulikuwa nayo wakati ukiwa hai, itaendelea kusemwa hata baada ya kuwa umeondoka hapa duniani.
Kitu cha pili ni tabia zako. Kama ulikuwa na tabia za kipekee, tabia zinazoendana na misingi muhimu, utakumbukwa hata baada ya kufa. Kama utakuwa mwaminifu na mwadilifu, watu watasema wazi kwamba mtu huyu alikuwa mwaminifu na mwadilifu, alisimamia alichoamini na alitimiza alichoahidi.
Ukiangalia vitu hivyo viwili, havihitaji uwe na mabilioni ya fedha, havihitaji uwe raisi wa nchi, wala havihitaji uwe na uwezo wa kipekee sana. Bali vinahitaji mtu uchague kuishi maisha yenye maana kwako na wale wanaokuzunguka. Uchague misingi ya maisha ambayo inaendana na sheria za sili na kuishi misingi hiyo.
SOMA; UKURASA WA 1000; Siku Elfu Moja (1000) Za Kuandika Kila Siku Bila Ya Kuacha Hata Siku Moja.
Na hakuna wakati mzuri wa kujenga jina lako zuri na tabia zako kama zama hizi. Kwa sababu sasa hivi kila mtu anajaribu kutafuta njia ya mkato ya kufanikiwa. Kila mtu anatafuta njia ya kuwalaghai wengine wampe kile ambacho anataka. na hili limetengeneza mazingira yasiyo ya uaminifu kwenye kila eneo la maisha yetu.
Ukiwa vizuri kwenye kile unachofanya, kwa kukazana kuwa bora kila siku, na ukawa na uadilifu kwenye maisha yako, ukaishi kwa misingi bila ya kuivunja, jina lako halitakufa, litaendelea kuishi milele.
Na wala hutasubiri mpaka ufe ndiyo jina lako liwe muhimu kwa watu, bali utaona matunda yake wakati bado upo hai. Utaona namna watu wananufaika kupitia wewe, utaona namna maisha yako yanakuwa na maana kubwa kwako na kwa wengine pia. Na hayo ndiyo tunasema ni maisha ya mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog