UKURASA WA 676; Vyanzo Vitano (5) Vya Uvivu Na Jinsi Ya Kuondokana Nao.

By | November 6, 2016

Uvivu na mafanikio ni vitu ambavyo haviwezi kwenda pamoja. Hakuna mtu mvivu aliyefanikiwa, na katika wengi wa walioshindwa, uvivu ni tabia ambayo wanayo.

Mafanikio yanakuhitaji ujitoe kuliko ilivyo kawaida. Yanakutaka uwe tayari kuweka juhudi kubwa zaidi ya unavyotaka kuweka. Unahitaji kuusukuma mwili wako hata pale unapohisi kuchoka.

Kiasili, sisi binadamu ni wavivu, hatupendi kujiumiza na hatupendi kuchosha miili na akili zetu. Hivyo mara zote tumekuwa tunatafuta njia rahisi ya kufanikiwa. Kwa kuwa njia hiyo haipo, wengi wamekuwa wakishindwa kufanikiwa.

Kama umekuwa na uvivu ambao unakuzuia kufanikiwa, ni vizuri kujua vyanzo vya uvivu huu na namna ya kuondokana na uvivu. Hapa tunakwenda kujifunza vyanzo vya uvivu na namna tunavyoweza kuondokana na uvivu.

1.     Afya ya mwili.

Kaa afya yako ya mwili haipo sawa, utakuwa na uvivu, hutaweza kufanya kazi zako kwa juhudi kubwa. Huwezi kufanya kazi vizuri kama unaumwa au kama kuna dawa ambazo unazitumia. Kwa sababu magonjwa na madawa yanauchosha mwili wako.

Ili kuondokana na sababu hii ya uvivu, hakikisha unailinda afya yako. Hakikisha unazuia magonjwa kabla hayajakufika.

2.     Vyakula unavyokula.

Vyakula unavyokula, vina mchango mkubwa kwenye nguvu ya mwili wako. Kama unakula vyakula vya sukari nyingi, mwili wako unachoka haraka na kushindwa kuweka juhudi kwenye kazi zako. Pia muda unaokula ni muhimu, kama unakula usiku sana kabla ya kulala, unaamka ukiwa umechoka na kuwa na uvivu. Kama unakosa kifungua kinywa, mwili unakosa nguvu ya kuweza kuianza siku yako vizuri.

Kuwa na uchaguzi sahihi wa vyakula unavyokula na wakati unaokula vyakula hivyo. Usile hovyo, usile vyakula vyenye sukari kwa wingi hasa kabla ya kazi. Pia usile usiku sana kabla ya kulala.

3.     Mazingira yanayokuzunguka.

Kama unazungukwa na mazingira ambayo yapo hovyo, na wewe unakuwa hovyo. Kufanya kazi kwenye eneo chafu, ambalo halijapangiliwa vizuri kunakuletea uvivu. Kufanya kazi kwenye eneo ambalo lina mwingiliano mkubwa wa watu na kelele, kunakuletea uvivu.

Kuondokana na hili, chagua mazingira sahihi kwako kufanya kazi. Mazingira yawe safi, mpangilio uwe mzuri kila unachohitaji kiwe kinapatikana. Punguza mwingiliano na kelele zisizo na msingi kwenye eneo lako la kazi.

4.     Watu wanaokuzunguka.

Kama umezungukwa na watu wavivu, nakuhakikishia na wewe utakuwa mvivu. Hii ni kwa sababu wale wanaotuzunguka wana mchango mkubwa wa pale tulipo. Kama wenzako hawafanyi, na wewe utajishawishi kwamba mpo pamoja na hivyo hufanyi. Mwisho unakuja kustuka kwamba upo nyuma kulingana na mipango yako mwenyewe.

Chagua kwa makini ni watu gani unaokuwa nao muda mwingi. Hakikisha hukai na watu ambao ni wavivu, watakuambukiza uvivu wao.

5.     Uchangamfu na ukakamavu wa mwili.

Hapa kuna vitu viwili, cha kwanza ni hali ya uchangamfu wa mwili, mwili wako unahitaji kuwa na uchangamfu ili kuweza kufanya kazi vizuri. Uchangamfu huu unaupata kama mwili wako umepeta muda wa kutosha wa kupumzika. Lazima upate muda wa kutosha wa kupumzika na kulala.

Kitu cha pili ni ukakamavu wa mwili, kama mwili siyo mkakamavu, utashindwa kuchukua hatua na hivyo kuwa mvivu. Kuondokana na hali hii fanya mazoezi mara kwa mara ili kuongeza ukakamavu wa mwili wako.

Uandae mwili wako na akili yako ili kuepukana na uvivu na uweze kuweka juhudi kubwa ili ufanikiwe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.