FALSAFA MPYA YA MAISHA; Uliza Kwanza, Ukamilifu Wa Kanuni Ya Dhahabu Ya Maisha Ya Mafanikio.

By | November 13, 2016

Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Ni siku nyingine nzuri kwetu wanafalsafa kukutana, kushirikishana yale muhimu ya kujenga falsafa ya maisha yetu ya mafanikio. Kumbuka lengo la falsafa yetu mpya ya maisha, siyo kujua falsafa ili tuwaringishie watu kwamba sisi ni wanafalsafa, badala yake ni kutuwezesha kuwa na maisha bora. Ni kujifunza hatua muhimu za kuchukua ili maisha yetu yaweze kuwa bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Ndiyo maana kila siku ya jumapili nakazana kukuandalia makala nzuri ya falsafa, ambayo kwa kuisomana kuifanyia kazi, unapata kitu cha kuyafanya maisha kuwa bora zaidi kila siku.

Jumapili iliyopita tulijifunza namna ya kutumia kanuni ya dhahabu kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kama unavyoijua kanuni ya dhahabu, ndiyo inayoendesha dunia, ndiyo inayotuwezesha kuendelea kuwa pamoja na kushirikiana kwenye jamii zetu. Bila ya kanuni ya dhahabu, dunia haiwezi kuwa sehemu nzuri na salama ya kuishi.

Makala ya leo ni mwendelezo wa kanuni ya dhahabu, kwa sababu kanuni ya dhahabu yenyewe isipotumika vizuri inaweza kuleta madhara makubwa kwa wengine. Hivyo leo tunakwenda kujifunza namna ya kuweka ukamilifu kwenye kanuni ya dhahabu, iweze kuwa kanuni bora kabisa ya kutuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

Kabla hatujaendelea, napenda nikujulishe kama hukupata nafasi ya kusoma makala iliyopita kuhusu kanuni hii ya dhahabu, basi isome kabla hujaendelea. Bonyeza maandishi haya kusoma makala iliyopita kuhusu kanuni ya dhahabu ili uweze kuwa na msingi mzuri wa kuelewa makala ya leo. Nikusihi sana, bonyeza hapa usome makala iliyopita ili uweze kuelewa makala ya leo.

Kama umeshasoma karibu sasa tuweke ukamilifu kwenye kanuni yetu ya dhahabu, ili tuweze kuitumia vizuri. Kama ambavyo tunaijua kanuni ya dhahabu, inasema kwamba WAFANYIE WENGINE KILE AMBACHO UNGEPENDA WAO WAKUFANYIE WEWE. Msingi wa kanuni hii ni kuwajali wengine pia, usijiangalie wewe pekee katika maamuzi unayofanya. Kitu ambacho ni kizuri sana kwa sababu mafanikio yetu yanatokana na wengine na siyo sisi wenyewe.

Lakini kanuni hii inaweza kutumika vibaya, hasa pale mtu anayeitumia anapokuwa hana mtazamo sawa wa maisha na mafanikio.

Kwa mfano kuna watu ambao wana mtazamo hasi juu ya maisha, kila kinachotokea wanakitafsiri kama kitu kibaya sana. Wanaona kama mwisho wa dunia umekaribia na hakuna namna mambo yanaweza kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa. kwa hali hii ya kukata tamaa, wanaweza kufanya mambo yanayoweza kuonekana sawa kwao wakati siyo sawa kwa wengine.

Kuna watu kutokana na maisha waliyopitia, na mambo waliyofanyiwa, wanaweza kuona kuwafanyia wengine ni sawa kabisa. Labda wao waliteswa na kunyanyaswa, na hivyo wanaona kunyanyasa na kutesa wengine ni sehemu ya maisha ya kawaida. Mtu aliyezoea kuiba kama sehemu ya kuongeza kipato, anaweza kuona ni sawa watu wakimwibia, lakini hili siyo sawa kwa watu wengi.

Na mwisho kabisa wapo watu ambao wamechagua mtindo wa maisha ambao unawafaa wao, lakini siyo sawa kwa kila mtu. Hivyo mtu anaweza kufanya kwa sababu kwake siyo shida, ila ikawa shida kubwa kwa wengine. Kwa mfano mtu ambaye anavuta sigara, haoni shida mtu kuvuta sigara mbele yake, kwa sababu yeye ni mvutaji. Sasa mtu huyu akitumia kanuni ya dhahabu, atakuwa sahihi kuvuta sigara mbele ya mtu mwingine yeyote, kitu ambacho kinaweza kuwa usumbufu na kero kubwa kwa wengine.

Swali ni je tunawezaje kuifanya kanuni ya dhahabu kuwa bora zaidi, ili tuweze kuitumia vizuri kila wakati na kwa kila mtu?

Na jibu ni ULIZA KWANZA. Kabla hujafanya jambo lolote kwa mtu yeyote, uliza kwanza. Muulize mtu huyo kwanza kama kile unachotaka kufanya ni sahihi kwake, au anakubaliana nacho. Kama anakubaliana nacho basi unaweza kufanya na wote mkawa kwenye wakati mzuri. Kama hakubaliani nacho basi unaacha kufanya na unaepuka kutengeneza migogoro isiyokuwa na msingi.

Uliza kwanza, popote na kwa yeyote unayekutana naye kwenye maisha yako. Usichukulie kwa sababu ni sahihi kwako basi itakuwa sahihi kwa kila mtu. Tuna uelewa na mitizamo tofauti, unaweza kufikiri unamsaidia mtu kumbe yeye anaona wewe ndiyo unamharibia zaidi.

Ukijijengea utamaduni wa kuuliza kwanza kabla ya kufanya, mara zote utakuwa upande sahihi wa kufanya mambo, utaweza kujenga ushirikiano bora na wengine na kuweza kupata mafanikio makubwa.

Kama tulivyojadili kwenye makala iliyopita, kanuni ya dhahabu tunaweza kuitumia kwenye kazi, biashara na hata maisha yetu ya kifamilia na kijamii. Hivyo basi kuuliza kwanza tunaweza kutumia kwenye kazi zetu, biashara zetu na hata maisha yetu kwa ujumla. Kwenye kila nafasi unayopata ya kumhudumia mtu, au kuwasiliana naye, usijaribu kufanya jambo linaloweza kuathiri maisha yake kabla hujamuuliza kwanza kama ni sahihi kwa upande wake.

Mara zote uliza kwanza, hasa kwa yale mambo ambayo hayajazoeleka kufanyika kwa wengi. Kuna mambo mengine unaweza kutumia uelewa wa kawaida kupata majibu, kwamba hata kama ni sahihi kwako, siyo kwa wote ni sahihi. Ila muhimu zaidi ni kuuliza kwanza pale unapotaka kufanya jambo ambalo huna uhakika kama mtu unayetaka kumfanyia litakuwa sahihi kwake.

Unapochukua nafasi ya kuwauliza wengine kwanza, wanaona ni heshima kubwa kwao na wanakuwa tayari kukupa ushirikiano wa kutosha kwa jambo lolote unalopanga kufanya, tofauti na unapoamua kufanya wewe mwenyewe.

Hivyo leo wanafalsafa wenzangu, tuongeze hili muhimu kwenye falsafa yetu mpya ya maisha, tukumbuke kuuliza kwanza kabla ya kufanya jambo lolote kwa wengine. Ni nafasi nzuri ya kujua watu wanataka nini hasa na kuhakikisha tunawapatia kile wanachotaka na ambacho ni sahihi kwao.

Falsafa mpya ya maisha kwa maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

kitabu-wakala

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: FALSAFA MPYA YA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.