UKURASA WA 700; Usifanye Chochote…

By | November 30, 2016

Mwandishi Elbert Hubbard amewahi kunukuliwa akisema kama hutaki kukosolewa, usiseme chochote, usifanye chochote na usiwe chochote. Hii ina maana kwamba kwa chochote utakachofanya, wapo watu watakaokukosoa, hata kama ni kitu kizuri kiasi gani. Kwa chochote utakachosema, wapo watu watakaokukosoa haijalishi umesema nini. Na vyovyote utakavyochagua maisha yako yawe, wapo watakaokukosoa. Hakuna anayeweza kukwepa hili.

Lakini bado watu wengi wamekuwa wakiogopa kukosolewa, na mimi nataka niongezee leo ya kwamba kama unachokwepa ni kukosolewa, usifanye chochote.

Lakini hasara ya kutokufanya chochote ni kubwa, kwa sababu huwezi kufanikiwa kama hufanyi chochote. Huwezi kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako kama hufanyi mambo mapya na makubwa. Na unapofanya mambo mapya na makubwa unakaribisha kukosolewa na kila mtu.

Ukweli ni kwamba huwezi kufanya jambo ambalo ni muhimu kwako halafu ukakwepa kukosolewa, japo ndivyo unavyotaka, lakini dunia haipo hivyo.

Watajitokeza watu kutoka kila kona na kukushauri njia bora ya kufanya. Watakuonesha kwa nini njia yako siyo sahihi au kwa nini utashindwa. Na wengi wanajikuta wakisikiliza kila anayekosoa na mwishowe kushindwa kupiga hatua.

Leo nataka nikupe siri ya kuweza kufanikiwa licha ya kukosolewa au hata kupingwa na wengi.

Suluhisho la hii ni hili;

Fanya kazi au kitu ambacho watu watakukosoa na kupinga, kama ndiyo kitu muhimu kwako kufanya, usijali kuhusu kukosolewa na kupingwa. Baada ya kufanya kazi hii kuwa na chujio la kuchuja ukosoaji unaoweza kufanyia kazi na mwingine ambao ni uchafu tu.

Sikiliza kwa makini wale wanaokosoa na jua kipi unachoweza kufanyia kazi, na kipi cha kupuuza. Kuna mambo machache sana unayoweza kuyafanyia kazi na yakakunufaisha, lakini mengine mengi ni uchafu tu, unakupotezea muda wako.

Usichukue kila ukosoaji unaotolewa, jua upi unakufaa na upi ni uchafu na kelele.

Kila mtu anapingwa na kukosolewa, hivyo usijione ni wewe tu unayeandamwa au kujifikiria kuna makosa makubwa unafanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.