Moja ya eneo gumu sana kwenye maisha yetu ya kila siku, ni watu kutuelewa na hatimaye kutuamini. Kuaminiana ndiyo kunaendesha kila kitu, kuanzia biashara, kazi na hata familia. Na ili watu wakuamini ni lazima kwanza wakuelewe kwa kile unachofanya au unachosema.
Lazima watu wakuelewe kwa aina ya biashara unayofanya na namna inavyoweza kuboresha maisha yao ndipo wakubali kuwa wateja wako.
Ni lazima mwajiri wako akuelewe kwa nini wewe unafaa kuwa mwajiri wake au kwa nini hatua fulani unayochukua ni muhimu.
Lazima ndani ya familia watu waelewane juu ya mambo ambayo kila mmoja anafanya au anapendelea kufanya.
Lakini uhalisia haupo hivi, watu wamekuwa hawaelewani kwenye mambo mengi na hivyo kushindwa kushirikiana na kufanikiwa kwa pamoja. Na mbaya zaidi pale ambapo mtu hajaeleweka, lawama zake anazipeleka kwa yule ambaye hajamwelewa, utasikia maneno kama;
Wateja wenyewe hawaelewi ubora na umuhimu wa bidhaa au huduma yangu.
Mwajiri wangu haelewi kwa nini ingekuwa bora sana kama ningefanya kitu fulani.
Mwenza wangu haelewi kwa nini tunahitaji kufanyia kazi wazo langu ambalo litatunufaisha baadaye.
Wazazi wangu hawanielewi ndiyo maana wanashindwa kuniunga mkono kwenye miradi ninayotaka kufanya.
Kwa kuanza; kama watu hawakuelewi basi hilo siyo kosa lao hata kidogo, bali linaweza kuwa kosa lako. Kwa sababu wewe ndiye uliyepaswa kuwaelewesha ili waelewe na wakuamini kisha muweze kushirikiana.
Kuna mambo mawili ambayo yanaweza kukusaidia watu kukuelewa kwa jambo lolote unalotaka kufanya na mkashirikiana vizuri.
Jambo la kwanza ni dhamira ya kweli.
Kama una dhamira ya kweli ya kufanya jambo, unayo nia hasa ya kuhakikisha jambo hilo linafanyika ili kupata matokeo bora, watu wataliona hilo ndani yako. Watajua ni kweli unamaanisha na watakuamini na kushirikiana na wewe.
Dhamira ya kweli haijifichi hata kidogo, inaonekana wazi wazi kwenye maneno na matendo ya mtu.
Jambo la pili ni mawasiliano ya wazi.
Hakuna kitu kinachoweza kujenga au kubomoa mahusiano ya aina yoyote ile kama mawasiliano. Mawasiliano yanapokuwa ya wazi na watu kujua kila kinachoendelea kwa wakati, wanaelewa na kuamini kile wanachoambiwa. Lakini kama mawasiliano siyo ya wazi, au hata hayapo kabisa, watu hawawezi kuelewa.
Watu wanahitaji taarifa sahihi juu ya jambo na kwa wakati sahihi. Watu wanataka kujua ni kipi hasa kinachoendelea na hatua zipi ambazo zinachukuliwa. Kwa mawasiliano ya wazi na kwa wakati, watu lazima watakuelewa.
Hivyo unahitaji DHAMIRA YA KWELI na MAWASILIANO YA WAZI ili uweze kueleweka na kukubaliana na mtu yeyote yule. Ukiona watu hawakuelewi, anza kuangalia mambo hayo mawili, je una dhamira ya kweli kwenye jambo hilo? Na je umewapa taarifa sahihi na kwa wakati sahihi? Mara nyingi kuna mahali patakuwa hapajakaa sawa kati ya hayo mawili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK