UKURASA WA 713; Jiambukize Mafanikio…

By | December 13, 2016

Mafanikio yanaambukizwa, na ndiyo maana kukaa karibu na watu waliofanikiwa, au kujifunza kupitia wao, unajiweka kwenye nafasi ya wewe kufanikiwa pia. Na kama ukikaa karibu na watu walioshindwa, au kujifunza kupitia wao, pamoja na kuwasikiliza, basi utaambukizwa kushindwa.

Pamoja na kwamba tunaambukizwa mafanikio kutoka kwa wengine, pia sisi wenyewe tunaweza kujiambukiza mafanikio. Na hii ni mbinu nzuri sana unayoweza kuitumia kupata hamasa ya kupiga hatua zaidi. Unaweza kutumia mbinu hii kufanya makubwa ambayo unaona kwa sasa hayawezekani.

Iko hivi kwa kawaida huwa tunaendelea kufanya kile ambacho tunafanya kwa wakati husika. Ndiyo maana kama umekaa na hufanyi kitu, basi utaendelea kukaa na kutokufanya kitu. Kama unaahirisha kufanya kitu, basi unajikuta unaendelea kuahirisha na kutokuchukua hatua. Hii pia inaashiria ya kwamba kama ukifanya kitu kidogo na ukafanikiwa, basi utakuwa umejiweka kwenye mwendo wa kufanikiwa.

Na hapa ndipo kujiambukiza mafanikio kunapoanzia.

Maana halisi ya kujiambukiza mafanikio ni kufanya kitu ambacho tayari upo vizuri kwenye kukifanya, halafu ukimaliza unafanya kile ambacho unataka kufanikiwa zaidi. Kwa kuanza na ushindi, basi unakuwa umejiweka kwenye hali ya kushinda na hii itakupelekea wewe kushinda zaidi na zaidi.

Kile unachoanza kufanya siyo lazima kiwe kikubwa sana, bali kinahitaji kuwa kitu ambacho unaweza kukifanya vizuri.

Kwa mfano, unapoamka asubuhi, unaweza kuchagua jukumu lolote dogo ambalo ukilifanya unajisikia umekamilisha kitu. Inaweza kuwa kufanya mazoezi, au kuamka mapema, au kucheza mchezo fulani. Inawezekana pia ikawa ni kufanya tahajudi, kukaa kimya kwa dakika kadhaa kutuliza akili yako.

Muhimu ni uwe na kitu unachokianza kabla ya kuanza jukumu lako kubwa la siku. Lakini pia kitu hiki kisichukue muda wako mwingi na kisiwe cha kukujengea ulevi. Mfano kama unatumia michezo ya kwenye kompyuta au simu (games) basi hakikisha haikupotezei muda na haikufanyi uwe tegemezi.

Kila siku hakikisha unaianza siku yako ukiwa na ushindi tayari. Kabla hujafanya jukumu lolote kubwa, anza na ushindi. Kwa njia hii utajiambukiza ushindi na mafanikio zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.