Hapo zamani, mababu zetu walizungukwa na madini ya kila aina, milima, maziwa na kila rasilimali muhimu. Lakini hawakujua thamani ya vitu hivyo mpaka pale walipokuja wakoloni na kuvichukua. Ndiyo maana utasikia mlima Kilimanjaro uligunduliwa na mzungu, sasa utajiuliza kuna watu wamekuwa wanakaa pembezoni mwa mlima ule miaka na miaka, ina maana walikuwa hawauoni?
Jibu ni kwamba walikuwa wanauona kila siku, ila hawakujua thamani yake, hawakujua kama ile ni fursa, na ndiyo maana hawakuweza kuutumia. Siyo kwamba wazee hawa walikuwa wajinga, ila tu hawakuwa na maarifa, ambayo yangewapa ufahamu na hatimaye kuweza kuiona fursa hiyo.
Sasa nataka nikuambie ya kwamba, habari hii haijaishia kwa wazee hao wa zamani. Bali inaendelea kwenye maisha yetu mpaka sasa. Umewahi kukaa mahali ukafikiria ufanye biashara gani na usione biashara ya kukufaa kufanya. Mara anakuja mtu anaanzisha biashara na inakuwa na mafanikio sana? Siyo kwamba wewe ni mjinga sana kuliko yule mwingine, ila tu umekosa maarifa, ambayo yangekupa ufahamu na hatimaye kuiona na kuweza kuitumia fursa.
Watu wanaimba fursa kila siku, lakini hawazioni, na hata wakiziona hawawezi kuzitumia. Hii ni kwa sababu wanaangalia kitu kimoja tu, fursa. Wakati ili fursa ikamilike, yaani uweze kuiona na kuitumia vizuri, unahitaji vitu viwili vya ziada. Hivyo kwa ujumla kuna vitu vitatu ambavyo vinakwenda pamoja.
Cha kwanza ni maarifa. Ni lazima uwe na maarifa na taarifa sahihi ndiyo uweze kuona fursa na hata kuzitumia. Bila ya maarifa utatembea juu ya dhahabu huku unalia na umasikini. Maarifa yanafungua macho yetu ya akili, na kutuwezesha kuona zaidi. Maana wanasema macho hayawezi kuona kila ambacho akili haijui.
Cha pili ni ufahamu au utambuzi. Unapopata maarifa na taarifa, zinakupa ufahamu wa kuweza kuelewa mazingira yako na yale yanayoendelea. Kujua tu hii ni dhahabu hakuwezi kukusaidia. Unahitaji kujua kwamba dhahabu ni madini adimu yanayotumika kwenye urembo. Unahitaji kujua mchakato wa kuyapata mpaka kuweza kuyauza. Unahitaji kujua mengi kuhusiana na fursa yoyote unayoiona.
Na cha tatu ndiyo fursa yenyewe sasa. Ukishakuwa na maarifa ambayo yanakupa utambuzi hapo ndipo unapoweza kuziona fursa na kuzitumia vizuri. Mchanganyiko huu ndiyo unaowawezesha baadhi ya watu kuona fursa kila mahali wakati wengine wanalalamika kila mahali.
Hapo ulipo zipo fursa nyingi mno zinazokuzunguka, huzioni kwa sababu hujajipa maarifa ya kutosha kukupa utambuzi wa mazingira yako.
Pata maarifa na taarifa bora kila siku, jijengee utambuzi na ufahamu wa mambo, na kila utakapopita utaziona fursa nyingi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK