Haijalishi ni mafanikio kiasi gani umeshapata mpaka sasa, ipo hatua ya juu zaidi ya hapo ulipofika sasa. Unaweza kuwa bora zaidi ya ulivyo leo, unaweza kupata fedha zaidi ya ulizonazo sasa, unaweza kupata elimu kubwa zaidi ya uliyonayo sasa. Unaweza kuwa na biashara kubwa na nyingi zaidi ya zile ulizonazo sasa.
Lakini wengi wanaishia kwenye mafanikio ambayo wameshayapata na kadiri muda unavyokwenda wanakuja kustuka kwamba wamerudi nyuma. Ukweli wa maisha ni kwamba kama huendi mbele basi unarudi nyuma. Hakuna kusimama, kama hufanyi chochote, basi umechagua kurudi nyuma. Kama hupigi hatua, basi unarudi nyuma.
SOMA; Hatua Sita Za Kuuchuja Ukweli Na Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuukaribia Ukweli.
Wengi hawajui kitu muhimu wanachopaswa kufanya ili kuweza kupiga hatua zaidi.
Unachohitaji ni hiki, kubali pale ulipo sasa, tambua hatua unayohitaji kufika na ijue hofu ambayo inakuzuia wewe kuchukua hatua.
Hivyo viwili vya kwanza tayari unavijua, tatizo kubwa linakuwa kwenye kuitambua hofu ambayo inakuzuia kupiga hatua kubwa zaidi.
Unapopata mafanikio kidogo, unakuwa unaogopa kuchukua hatua ambazo huna uhakika nazo kwa hofu ya kurudi kule ambapo umetoka. Sasa hofu hii ndiyo inakuzuia kuchukua hatua na mara nyingi unajikuta unarudi nyuma.
Unachohitaji kufanya ni kutambua hofu unayoipata ni hali ya kawaida na ili uweze kufika hatua ya juu zaidi ya hapo ulipo sasa, ni lazima uchukue hatua licha ya hofu uliyonayo sasa. Unapaswa kuelewa hofu hiyo ni tahadhari kwako kuwa makini ili uweze kupata matokeo bora.
Usikubali hofu ikuzuie wewe kuchukua hatua, itumie hofu kama kichocheo cha kupiga hatua zaidi. Usibaki hapo ulipo, piga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK