Ili uweze kufanikiwa kwenye maisha yako, unahitaji kuwa kiongozi bora. Unahitaji kuweza kujiongoza wewe mwenyewe na hata kuwaongoza wengine pia.
Watu wengi wanaposikia uongozi moja kwa moja hupeleka mawazo yao kwenye nafasi za kisiasa, au vyeo kwenye kazi na nafasi nyingine za kijamii, lakini hiyo siyo maana halisi ya uongozi.
Uongozi ni pale mtu anapofanya jambo, na wengine wanavutiwa kumfuata, kumsikiliza na kufanya kile ambacho anafanya.
Sasa utagundua kwa nini unahitaji kuwa kiongozi ili ufanikiwe, kwa sababu kama unafanya biashara, basi unahitaji watu wanaokusikiliza, kukufuata na kufanya kile ambacho unataka wafanye. Na hawafanyi kwa sababu yako, bali wanafanya kwa sababu zao binafsi. Kama ambavyo unasoma hapa, husomi kwa sababu nimeandika, ila unasoma kwa sababu unahitaji kupata maarifa yatakayokuwezesha kupiga hatua zaidi.
SOMA; Sifa Kuu Ya Uongozi Unayotakiwa Kuwa Nayo…
Kila eneo la maisha yako, unahitaji kuwa na tabia za uongozi, unahitaji kuwa kiongozi mzuri ili watu waweze kukufuata na kukusikiliza.
Watu wamekuwa wakijiuliza iwapo viongozi wanazaliwa au wanatengenezwa. Yaani kama mtu anazaliwa akiwa na tabia za uongozi, au mtu yeyote anaweza kujifunza na kuwa kiongozi. Na jibu bila ya kubabaisha ni kwamba mtu yeyote anaweza kujifunza na kuwa kiongozi. Na leo hapa nakwenda kukupa siri moja ya uongozi, ambayo kama utaweza kuitumia basi utapiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Siri kuu ya uongozi ni hii; FANYA KILE UNACHOAMINI.
Soma hayo maneno vizuri, kuna neno FANYA ikiwa na maana vitendo na siyo maneno. Na pia kuna neno IMANI, ikiwa na maana kwamba una uhakika na kile ambacho unafanya na kusimamia kwamba kinaendana na vile unavyoyachukulia maisha na upo tayari kusimamia hilo.
Ukiweza hayo mawili, kufanya na kuwa na imani, watu watakuwa tayari kukufuata kwa kile unachotaka wafanye. Kwa kuwa unapofanya, unawavutia wengi kuliko kuongea. Kila mtu anaweza kuongea na maneno yanawachosha watu. Vitendo ni adimu na vitu adimu vinawavutia wengi. Unapoamini kwenye kile unachofanya, unawafanya na wengine pia waamini na kukuamini wewe. Unapokuwa na maono makubwa ya mbeleni na kuyasimamia, watu watakuwa tayari kwenda na wewe, ili wawe sehemu ya maono hayo makubwa.
Fanya kile unachoamini, na watu watakuwa tayari kuongozana na wewe, popote pale unapoelekea.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK