Je utajuaje kama misingi unayofuata kwenye kazi zako, biashara zako na hata maisha yako kwa ujumla ni misingi sahihi? Hili ni swali ambalo watu wengi wamekuwa hawapati nafasi ya kujiuliza na hivyo kupelekea kujikuta wakifuata misingi ambayo siyo sahihi na baadaye kuanguka.
Watu wengi wamekuwa hawajiulizi swali hili kwa sababu wamekuwa wanaichukua misingi katika wakati ambao ni mzuri, nyakati zinapobadilika na misingi hiyo kushindwa kuwasaidia, wanajikuta wakianguka pale misingi inapoanguka.
SOMA; UKURASA WA 734; Kipimo Cha Misingi Sahihi Kwako…
Kwa mfano, siku za nyuma kidogo kwa hapa Tanzania watu walikuwa wakiambiana na kuamini kabisa ya kwamba kufanya biashara kwa kufuata sheria huwezi kufanikiwa. Hivyo watu wakaamini na kutafuta njia zisizo za kisheria za kufanya biashara. Wakawa na njia za kukwepa kodi, kupata faida kwa udanganyifu na hata kuiba. Lakini uongozi umebadilika na mambo yamebadilika, wale waliotegemea misingi hiyo wamekuwa wanaumia kila siku.
Swali letu ni je nitajuaje kama msingi ninaofuata mimi ni sahihi?
Kujibu swali hili kwanza tuangalie msingi tuliozoea, tuangalie msingi wa nyumba. Kama unajenga nyumba, au unaishi kwenye nyumba, unajuaje kama msingi wa nyumba ni sahihi? Kitu cha kwanza kuangalia ni uimara, na uimara huu unaupima kwa nyakati. Lazima msingi uwe imara kwa nyakati zote, wakati wa jua, wakati wa mvua na wakati wa upepo. Na kadiri tunavyokwenda, pia msingi uwe imara wakati wa tetemeko. Hapa ndiyo unaweza kuwa na amani kwamba upo kwenye msingi sahihi.
SOMA; Misingi Mikuu Miwili Ya Kukuza Biashara Yoyote Ile.
Hivyo hivyo kwenye misingi yako ya maisha, msingi sahihi ni ule unaosimama nyakati zote, wakati mambo ni mazuri na wakati mambo ni mabaya au kuna changamoto. Kama msingi unafanya kazi wakati mzuri na kushindwa wakati mbaya, huo siyo msingi sahihi. Kwa sababu kwenye maisha tunapitia nyakati zote nzuri na mbaya.
Misingi yako ya kikazi, kibiashara, kifedha na kimaisha kwa ujumla, lazima uweze kuitegemea kwa kila nyakati unazopitia. Hata kama kuna changamoto kubwa, msingi uweze kukusimamisha.
Chagua misingi ambayo imedhibitishwa kuwa imara kwenye nyakati nzuri na nyakati mbaya na itakuwezesha kuendesha maisha yako vizuri na kwa mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK