Hakuna siku ambayo inaweza kupita na usiwe na changamoto yoyote kabisa. hata kama itakuwa siyo kubwa basi inaweza kuwa ndogo. Mfano unataka kuwahi mahali halafu njiani ukakuta foleni ni ndefu na hivyo usiweze kufika kwa wakati. Au kuna mtu ulitegemea atimize wajibu wake na yeye hajatimiza.
Kwa asili binadamu tunaona changamoto hizi kama kikwazo kwetu na kuziona ndiyo zinatuzuia kufanikiwa. Lakini hii siyo kweli, ninachoweza kukuambia ni kwamba bila ya changamoto huwezi kufanikiwa. Changamoto ni sehemu muhimu ya mafanikio.
SOMA; Changamoto Za Kuondoka Kwenye Vifungo Vya Maisha Na Kupata Uhuru Wa Maisha.
Ni changamoto ndizo zinazotufanya tuweze kufikiri zaidi, tuhoji zaidi na kuweka juhudi zaidi. Ni changamoto zinazotufundisha namna bora ya kwenda na watu. Na pia ni changamoto zinazotukumbusha kutokuwa na mategemeo makubwa kwenye mambo ambayo hayapo chini ya udhibiti wetu.
Umeshawahi kuona mfano wa mtu ambaye amekuwa kwenye ajira kwa muda mrefu huku maisha yake yakiwa magumu, mara inatokea anapoteza ajira ile, lakini baada ya kuipoteza anajikuta akiweza kufanya makubwa na kufanikiwa zaidi? Hii ni moja ya njia ambazo changamoto inamsukuma mtu kufanya makubwa zaidi.
Unakuta mtu anaendesha maisha yake kwa mazoea, hata kama ni magumu, lakini inapotokea changamoto na kumlazimisha kubadilika, ndipo anagundua uwezo wake mkubwa na kuweza kufanya makubwa.
SOMA; Changamoto Nyingine Ya Kusema Ukweli…
Changamoto ndiyo kichocheo cha ugunduzi wa teknolojia mbalimbali tunazozifurahia sasa, mtu ambaye hana changamoto yoyote, hakuna kitakachomsukuma kuchukua hatua.
Hivyo rafiki, unapokutana na changamoto, badala ya kuanza kulalamika kama wengine, wewe kaa chini na jiulize unanufaikaje na changamoto unayopitia. Angalia ni namna gani unaweza kuboresha zaidi ili usiingie kwenye changamoto kama hiyo tena. Na wakati mwingine unapotatua changamoto yako, unaweza kuwasaidia wengine nao wakatatua changamoto zao na wakawa tayari kukulipa.
Changamoto ni hamasa kwako kufanya makubwa zaidi, itumie kila changamoto vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK