UKURASA WA 751; Watu Wenye Ushawishi Mkubwa Kwako Ni Hawa…

By | January 20, 2017

Kuna usemi maarufu sana ya kwamba wewe ni wastani wa wale watu watano unaokuwa nao kwa muda mwingi, wale watu watano wanaokuzunguka ndiyo wenye ushawishi mkubwa sana kwako.

Kama utazungukwa na wezi watano, basi moja kwa moja na wewe utakuwa mwizi. Kama utazungukwa na wavivu watano, wewe utakuwa mvivu wa sita. Kama utazungukwa na masikini watano, basi jumla kutakuwa na masikini sita.

Ni rahisi kujua hili lakini kulielewa kwa ndani ndiyo changamoto. Ni changamoto kuelewa kwa sababu tumekuwa tunajidanganya kwamba tunaweza kukaa na watu wenye tabia fulani na tusiige tabia zao, tunajidanganya kwamba sisi ni wajanja sana na hivyo hatuwezi kuathiriwa na tabia za wale wanaotuzunguka.

SOMA; Tumia Nafasi Yako Ya Kuchagua Vizuri…

Unakumbuka wakati ukiwa mdogo, wazazi wako walikukataza kukaa na watoto fulani kwa sababu wana tabia mbaya, au alikunyima kujiunga na vikundi fulani vya watoto au vijana kwa sababu tabia zao siyo nzuri. Wewe uliona kama anakunyima haki ya kuwa na marafiki, kwa sababu uliamini kwamba unaweza kukaa nao lakini usichukue tabia zao. Nafikiri sasa utakuwa na uzoefu kama uliwafuata au hukuwafuata, utakuwa umeyaona matokeo.

Sasa hali ile haikuishia utotoni, mpaka sasa bado ipo na madhara yake bado yanaendelea kwako. Wale watu unaokuwa nao muda mrefu, wale wanaokuzunguka muda mwingi, wana ushawishi mkubwa kwako, wana mchango mkubwa sana wa hapo ulipo sasa.

Na hii siyo kwa sababu wanakulazimisha, bali ni asili yetu sisi binadamu. Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, tunapenda kukubalika ndani ya jamii fulani ambayo tupo. Na ili tukubalike tunahitaji kufanana na jamii hiyo, tunahitaji kufanya yale ambayo wanafanya, ili tuwe pamoja. Ndiyo maana ukijiangalia hapo ulipo sasa, na ukiangalia marafiki zako wa karibu, hamtofautiani sana. Wote mtakuwa mnafanya mambo yanayofanana, mna mafanikio yanayofanana na mna mwelekeo unaofanana.

Ninachotaka kukukumbusha hapa leo rafiki yangu, ni sawa na kile wazazi wako walikuwa wanakuambia wakati unakua. Angalia sana wale watu ambao unakaa nao muda mwingi, angalia sana wale watu ambao ni marafiki zako. Kama wana tabia ambazo huzipendi, au haziendani na misingi ya mafanikio, ni wakati wa wewe kuchukua hatua kwa sababu kuendelea kuwa nao utazikaribisha tabia zao kwako.

Changamoto nyingine hapa ni kwamba kama tayari umekaa na watu hao muda mrefu, maana yake umeshabeba tabia zao na hivyo huwezi kuziona tena.

Hivyo unaweza kukaa chini leo na kufanya tafakari ya maisha yako, kuona namna ambavyo umekuwa unafanya mambo yako na imani uliyonayo juu ya maisha, kama unaona haviendani na maisha ya mafanikio, badilika mara moja na badili wale unaokuwa nao muda mrefu.

Na kama huna watu wazuri wa kuwa nao muda mrefu, ambao watakuhamasisha kuwa na maisha ya mafanikio, basi chagua watu waliofanikiwa na jifunze kupitia wao, soma vitabu vyao, angalia namna walivyokuwa wanaendesha maisha yao. Hii itakuwa afadhali kuliko kuendelea kuwa na wale ambao wanakurudisha nyuma.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.