Kama umewahi kuwa mfuatiliaji wa masoko ya hisa, hasa ya nchi za nje kama marekani, utakuwa unaelewa tabia ya soko la hisa ni kupanda na kushuka. Yaani kauli moja tu ya kiongozi inaweza kupandisha au kushusha hisa za makampuni fulani. Mabadiliko kidogo kwenye maisha yanaweza kuleta kupanda au kushuka kwenye hisa.
Sasa hili haliishii kwenye hisa pekee, bali ndiyo asili ya maisha, kuna kupanda na kushuka. Wakati mwingine kunakuwa kwa kiasi kikubwa, wakati mwingine kunakuwa kwa kiasi kidogo. Ni hali ya kawaida kabisa, na kila mwanamafanikio lazima ajue hili na namna ya kwenda nalo.
Ni asili ya binadamu kupenda kuwa juu wakati wote, tunapenda kupanda wakati wote, hivyo ikitokea tumeshuka au tupo chini, basi tunataharuki na kuona mambo yanakwenda mrama. Unaweza kuona hili kwenye hayo hayo masoko ya hisa, pale hisa zinaposhuka, wasiojua wanakimbilia kuuza, wakiona ni hasara, sasa wengi wanapouza bei inashuka zaidi na zaidi. Na hapa ndipo wale wanaojua wanaponunua kwa wingi na baadaye soko linapotulia, na lazima litulie, watu wanaanza kununua tena, bei zinapanda na wale walionunua wakati kila mtu anauza, wanauza kwa faida nzuri.
Unahitaji kulielewa hili vizuri kwenye maisha yako, kwa sababu pale mambo yanaposhuka, kama ambavyo huwa yanashuka, ndiyo wakati unaohitaji kukaa chini na kutafakari kwa kina, ndiyo wakati ambao unahitaji kuwa mtulivu na kujua hatua zipi sahihi kuchukua. Ukitaharuki na kuchukua hatua za hovyo, utaendelea kujizamisha zaidi.
SOMA; Usipigane Na Usichokitaka Na Jinsi Ya Kupata Unachotaka.
Pale mambo yanaposhuka, jua ni kwa wakati tu, yatapanda tena, na pia yanapopanda jua ni kwa wakati, yatashuka pia. Lakini sasa usifikirie hivyo halafu ukakaa chini kusubiri mambo yakae sawa, badala yake unahitaji kuendelea kuweka juhudi kubwa sana, unahitaji kuendelea kufanya kazi sana ili kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri.
Kuepuka kuumizwa pale mambo yanaposhuka, usijishikize na kitu chochote, usikubali kutambulika kwa vitu, maana pale vitu hivyo vinapoondoka, utaona utambulisho wako unapotea. Jitambulishe wewe kama wewe, kwa utu wako na siyo kwa cheo, ambacho unaweza kukipoteza muda wowote au kwa mali ambazo zinaweza kupotea muda wowote.
Kuwa mtulivu kwenye kila hatua ya maisha yako, hakuna kinachodumu milele. Jambo lolote, tiba yake ni muda. Chukua hatua sahihi, fanya kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako kufanya, na mambo yatakwenda vizuri kadiri muda unavyokwenda. Haijalishi unapitia changamoto au magumu kiasi gani, kama bado upo hai, hujafika mwisho, mambo mazuri zaidi yanakuja.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK