UKURASA WA 759; Kila Kitu Kinaweza Kuwa Bora Zaidi…

By | January 28, 2017

Wanasema mafanikio ni nguvu asilimia 10 na mtazamo asilimia 90, na hii ni kweli kabisa. Kwa sababu hakuna kitu kinachowarudisha watu nyuma kama mtazamo. Kile kitu ambacho watu wanakiamini na kukiishi kwenye maisha yao ya kila siku, ndiyo kikwazo namba moja kwa mafanikio yao.

Tafiti nyingi mno zimefanywa juu ya watu ambao wanabahatika kupata fedha nyingi kwa haraka, labda kwa kushinda bahati nasibu, lakini baada ya muda wanarudi kwenye umasikini wao. Na majibu yote yanarudi kwenye mtazamo, imani na tabia ambazo watu wanazo linapokuja swala la fedha.

Wapo watu wengi ambao wamenasa kwenye madeni, siyo kwa sababu  walikuwa na umuhimu wowote wa madeni hayo, ila kwa sababu mtazamo walionao juu ya fedha unawapelekea kujikuta kwenye madeni. Wao wanachofikiria ni kwamba wanataka fedha na wanazitaka sasa, na kama hawana, basi watakopa na kupata fedha hizo.

Sasa tofautisha huyo anayetaka sasa hata kwa kukopa na yule ambaye anataka fedha, ila anajiambia lazima afanye kitu kitakachomwezesha kuzalisha ile fedha anayoitaka. Moja kwa moja huyu mwenye mtazamo wa kuzalisha, atapiga hatua zaidi, wakati mwenzake akiwa anajichimbia shimo la kuzama kwenye madeni.

Sasa leo nakwenda kukukumbusha mtazamo muhimu sana wa maisha ambao tunapaswa kwenda nao kwenye maisha yetu ya kila siku. Kwa kuwa na mtazamo huu, hutajikuta ukiwa na msongo wa mawazo wala kukata tamaa, kwa sababu kila gumu unalopitia, utaona njia mbele.

SOMA; Acha Kuishi Falsafa Hizi Ambazo Zinakuzuia Kuishi Maisha Bora Na Ya Furaha.

Mtazamo huu muhimu ni kila kitu kinaweza kuwa bora zaidi ya kilivyo sasa. KILA KITU.

Kwa kuanza na wewe mwenyewe, unaweza kuwa bora zaidi leo kuliko ulivyokuwa jana, na unaweza kuwa bora zaidi kesho kuliko ulivyo leo.

Kazi yako inaweza kuwa bora zaidi ya vile ilivyo sasa.

Biashara yako inaweza kuwa bora zaidi ya hapo ilipo sasa.

Afya yako inaweza kuwa bora zaidi ya vile ilivyo sasa.

Na hata familia yako inaweza kuwa bora zaidi ya ilivyo sasa.

Lakini sasa, ubora huu hauji tu wenyewe kama ajali, bali unaletwa. Utaweza kuwa bora zaidi kama utachagua kuwa bora zaidi na utaweka juhudi kuhakikisha unakuwa bora zaidi.

Kwenye kila unalofanya kwenye maisha yako, hii iwe imani yako, huu uwe mtazamo wako na pia iwe tabia yako. Kwamba unaweza kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa, hivyo unahitaji kuweka juhudi zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.