UKURASA WA 760; Siyo Mara Moja, Ni Kila Mara…

By | January 29, 2017

Tangu umezaliwa mpaka hapo ulipo sasa, kila siku unakula, jana ulikula, leo umekula na kesho utakula, hatuna shaka juu ya hilo.

Siku zote za maisha yako umekuwa unaufanyia usafi mwili wako, na kila siku utaendelea kufanya hivyo, utaoga na kusafisha nguzo zako, ni maisha ya kila siku, siyo kitu cha kufikiria kwamba utafanya au la.

Lakini sasa inapokuja kwenye mafanikio, utawashangaa watu wanafanya kidogo halafu wanafika mahali na kuacha.

Au inapokuja swala la kujifunza, mtu anasoma kitabu kimoja na kuona tayari ameshajua kila kitu. Au anapata shahada moja na kufunga kabisa vitabu.

SOMA; Mipango Siyo Matumizi…

Leo nataka nikukumbushe hili, maana wengi wamepotezwa.

Mafanikio ya maisha ni kitu ambacho tunafanya kila siku, siyo mara moja moja, siyo unapojisikia, bali ni kitu cha lazima kufanya kila siku.

Huamki asubuhi na kuanza kujiuliza leo utakula au la, ni pale njaa inapokuja na utatafuta kitu ule. Mafanikio pia ndivyo yalivyo, ikiwa huna njaa kila siku na kila mara, hutaweza kupiga hatua.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kujifunza, kila siku lazima ujifunze, haijalishi unajua kiasi gani, bado vipo vingi vya kujua zaidi na zaidi, hivyo kujifunza ni zoezi la kila siku, kama ilivyo kula na kuoga.

Ndiyo maana moja ya mambo nilikushauri ufanye mwaka huu 2017, ni kuwa na mfumo wa maisha ambao utaufuata kila siku. Yaani kila siku unapoamka unajua nini unakwenda kufanya, siyo mjadala wa ufanye au usifanye, unaamka na kufanya. Kufanya mazoezi, kujifunza na hata kazi zako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.