Maneno matatu yanayoweza kubeba mafanikio yako yote kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla.
Unaanza na hadithi, hii ni ile ndoto yako kubwa ya maisha, ni yale maono unayoyapata ya namna unataka maisha yako yawe. Nimewahi kukuambia tena ya kwamba maisha ni hadithi, hivyo ni uamuzi wako unataka kuishi hadithi gani, unaitengeneza na kuanza kuiishi. Kwa bahati mbaya sana tunaingia kwenye jamii ambazo zipo hadithi za watu wengine, na tunaaminishwa kwamba hizo ndizo hadithi nzuri kuziishi. Hivyo hatua ya kwanza kabisa ni kutengeneza hadithi yako, au kuiboresha zaidi ili iweze kuendana na maisha uliyochagua.
SOMA; Unapimaje Ushindi Kwenye Maisha Yako?
Baada ya hadithi unakuja mchezo, maana hadithi ni jambo moja, kufikia hadithi au ndoto yako ni jambo jingine muhimu. Unahitaji kuwa na njia za kufika kwenye yale maisha ya ndoto yako, maana haitatokea yenyewe kama ajali. Kuna namna unahitaji kuishi maisha yako ya kila siku, ili kuweza kuifikia hadithi yako. Hivyo unahitaji kutengeneza mchezo wako, wa namna gani unaianza siku yako, namna gani unafanya mambo yako, kipi unafanya na kipi hufanyi. Tengeneza mchezo wako, au boresha ule ulionao sasa.
Mwisho ni ushindi, unapimaje ushindi kwenye mchezo wako wa kufikia hadithi yako. Kila mchezo unapimwa kwa ushindi, siyo kwa chenga bali kwa ushindi. Ili uweze kuendelea na mchezo unahitaji hamasa ya ushindi, hatua ndogo ndogo nzuri unazopiga kila siku ili kufikia ndoto yako. Kadiri unayopiga hatua nzuri, unapata hamasa ya kuendelea zaidi.
Hadithi, mchezo na kisha ushindi, hatua tatu muhimu za kupitia kila siku. Kila unapoamka jikumbushe hadithi yako, pitia ndoto zako na maono yako makubwa ya maisha. Kisha pitia mchezo wako, anza kufanya yale muhimu. Na mwisho wa siku hesabu ushindi wa siku yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK