UKURASA WA 766; Ondoka Kwenye Gereza La Kibiashara….

By | February 4, 2017

Watu wengi wanapoingia kwenye biashara, wanakuwa na ndoto kubwa sana, wengi wanaona wanakwenda kuwa huru kuweza kufanya kile ambacho wanataka kufanya.

Hata wale wanaoondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri au kuanzisha biashara zao, hufikiri kwamba wanakwenda kuwa huru kufanya chochote wanachotaka.

Huu siyo uhalisia, mwanzoni mwa kila biashara, mmiliki wa biashara anajikuta akifanya mambo mengi yeye mwenyewe. Kila kitu kinamtegemea yeye na ule uhuru waliokuwa anaufikiria hauoni tena. Anakuwa ameingia kwenye gereza jipya. Kama ajira ilikuwa gereza ambalo yeye alikuwa mfungwa na mwajiri alikuwa msimamizi, sasa anakuwa ameingia kwenye gereza ambalo yeye mwenyewe ndiye mfungwa na yeye mwenyewe ndiye msimamizi wa mfungwa huyo.

Wengi wanabaki kwenye hali hii na kuendesha biashara zao zikiwa ndogo kwa muda wote na wanashindwa kupata mafanikio makubwa kibiashara.

SOMA; Utumwa Wa Kujinunulia Mwenyewe…

Jambo moja muhimu unapaswa kujua ni kwamba huwezi kufanikiwa kwenye biashara kama unafanya kila kitu peke yako, kama kila kitu unafanya wewe mwenyewe, hutabaki na nguvu na muda wa kukuwezesha kufanya yale muhimu.

Hivyo wito hapa ni kwa kila mwanamafanikio kuhakikisha ananunua uhuru wake, ili aweze kuwa huru kufanya yale yatakayompeleka kwenye mafanikio zaidi. Unahitaji kuwa na wasaidizi, kwenye kila kitu unachofanya, kama yupo mtu anayeweza kukifanya vizuri, na kwa gharama ndogo kuliko unazopoteza wewe kwa kukifanya, basi tafuta mtu akusaidie kufanya.

Kila siku pigana kununua uhuru wako, kwa kupata watu wa kukusaidia ili uweze kufanya makubwa zaidi. Biashara yako haiwezi kukua kama akili yako itakuwa inafikiria mambo madogo madogo ya kila siku kwenye biashara.

Ondoka kwenye gereza la kibiashara kwa kuhakikisha unapata wasaidizi wa kutosha kwenye maeneo yote muhimu ya biashara yako, na wewe unafanyia kazi yale ambayo ni muhimu zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.