UKURASA WA 772; Kumbuka Rasilimali Ulizonazo…

By | February 10, 2017

Wanapokutana na changamoto, watu wengi husahau ya kwamba kuna rasilimali ambazo tayari wanazo. Wanaona changamoto ile ni tatizo kubwa kwao ambalo hawawezi kulitatua. Wanasahau kwamba tayari wanazo rasilimali nyingi zinazowazunguka, wanazoweza kuzitumia kupiga hatua zaidi.

Hapo ulipo unazo rasilimali nyingi ambazo zinaweza kukuvusha popote unapojikuta.

Rasilimali hizo zinaanza na wewe mwenyewe kwa ule ujuzi ulionao, uzoefu ulionao, uwezo wako mkubwa, vitu unavyomiliki na hata hamasa yako binafsi. Hivi ni vitu ambavyo ukiweza kuvitumia vizuri unaweza kuvuka changamoto yoyote unayokutana nayo.

Rasilimali nyingine ni zile zinazotuzunguka, watu wanaotufahamu, mazingira tuliyopo, mahusiano yetu na wengine na hata kazi au biashara ambazo tunafanya. Kila kitu kinachokuzunguka, iwe ni watu au vitu vya kawaida, ni rasilimali muhimu kwako kukuwezesha kutoka pale ulipo sasa.

SOMA; Rasilimali Mbili Muhimu Unazohitaji Ili Kuwa Bora…

Tatizo kubwa tunapokutana na changamoto, akili zetu zinataharuki, tunasahau kila kitu na akili zetu zote zinakuwa kwenye ile changamoto. Changamoto hiyo inatufumba kabisa macho na hatuoni tena tunawezaje kutumia rasilimali zinazotuzunguka.

Ni sawa na mchezaji ambaye yupo uwanjani, ana presha kubwa ya kutaka kufunga goli kwa sababu timu yake ipo nyuma, anafika na mpira golini, anasahau kwamba kuna mchezaji mwenzake yuko pembeni na yupo kwenye nafasi nzuri ya kufunga, anakazana kufunga yeye, anajikuta ametoa mpira nje ya uwanja.

Tumekuwa tunafanya hivi kila siku kwenye maisha yetu, changamoto au matatizo yanatufanya tushindwe kuona nafasi nzuri za kuchukua badala yake tunafanya makosa zaidi.

Hatua za kuchukua, pale unapokutana na changamoto au tatizo lolote, usiruhusu akili yako itaharuki, usikimbilie kuchukua hatua. Badala yake kaa chini na fikiri changamoto ile kwa kina, angalia tatizo hasa ni nini na linatatuliwaje. Baada ya hapo angalia rasilimali ulizonazo na namna unavyoweza kuzitumia kutatua changamoto hiyo. Kila ulichonacho na kila kinachokuzunguka ni rasilimali, angalia unawezaje kuitumia kwenye changamoto hiyo.

Kwa kufuata haya, utaona njia bora za kutatua kila changamoto unayokutana nayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.