Ukisimama mbele ya watu na kusema wewe ni mbinafsi, watakuangalia vibaya na kukuchukulia wewe ni mtu mbaya, usiyejali wengine. Hii ni kwa sababu ubinafsi umepewa picha ambayo siyo nzuri. Hasa pale unapohusishwa na fedha au mali, mtu mbinafsi anaonekana kuwadhulumu wengine ili yeye apate zaidi.
Lakini tupo hapa tulipofika binadamu kwa sababu ya ubinafsi. Upo ubinafsi mzuri na upo ubinafsi mbaya. Ubinafsi mzuri ndiyo unajenga jamii bora, yenye ushirikiano mzuri na mafanikio makubwa. Ubinafsi mbaya ndiyo unaoharibu jamii, kuleta mapigano na kuharibu mahusiano.
Ubinafsi mbaya najua unaujua, na kama umesahau basi ni pale unapokazana kupata wewe kwanza hata kama wengine wanaumia, unajifikiria wewe mwenyewe tu bila ya kujali wengine. Kwa njia hii unaweza kupata unachotaka, lakini wengine wataumia.
Ubinafsi mzuri ni pale unapoyajua yale muhimu kwako wewe kwanza, na kuhakikisha yapo vizuri ili uweze kuwasaidia wengine pia.
Kwa mfano huwezi kuwasaidia wengine hata kama unawajali kiasi gani ikiwa una afya mbovu. Kama umelala kitandani kwa ugonjwa, wewe utahitaji msaada zaidi kuliko hata wale unaotaka kuwasaidia.
Pia kama wewe ni masikini, hutaweza kuwasaidia wale wengine wenye uhitaji, hivyo unahitaji kuweka hali yako ya kifedha sawa ili kuweza kuwa na msaada kwa wengine.
SOMA; Ubinafsi Wa Maisha Na Unavyokuzuia Kuwa Na Maisha Bora.
Kuchukua muda wako na kuwekeza kwenye afya yako binafsi ni ubinafsi mzuri kwako, kula vizuri, kufanya mazoezi na kujilinda na magonjwa ni kitu kitakachokusaidia wewe na wengine pia.
Kuweka juhudi zaidi kwenye kile unachofanya, kuwa mbunifu zaidi, kujitoa zaidi ni ubinafsi mzuri ambao utakuwezesha kuongeza kipato chako na kukaa mbali na umasikini. Na kwa kutokuwa masikini utakuwa umeweza kuwasaidia wengi, hata kuwaonesha tu ya kwamba inawezekana.
Kumbuka huwezi kutoa kitu ambacho wewe mwenyewe huna, hivyo kuwa mbinafsi mzuri kwa kuhakikisha unakwenda hatua ya ziada kupata vile ambavyo ni muhimu na vitaweza kuwasaidia wengine zaidi. Hatua ya kwanza ya kuwasaidia masikini, ni wewe kutokuwa masikini. Halafu mengine yanaweza kufuata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK