UKURASA WA 805; Vipi Kama Ukipunguza Nusu..?

By | March 15, 2017

Ipo sheria ya ufanisi ambayo inaitwa sheria ya Pareto au Pareto Principle. Jina jingine la sheria hii ni 80/20. Sheria hii inasema kwamba asilimia 80 ya matokeo inasababishwa na asilimia 20 ya juhudi unazoweka. Yaani kama kuna vitu kumi unavyofanya, vitu viwili vinaleta matokeo makubwa kuliko vile vitu vingine nane unavyofanya, ukivikusanya pamoja.

IMG-20170218-WA0001

Sheria hii pia inatumika kwenye biashara, kwamba asilimia 20 ya wateja wako wanaleta asilimia 80 ya faida yote. Au asilimia 20 ya vile unavyouza ndiyo inaleta asilimia 80 ya faida yote. Unaweza kuitumia sheria hii kwenye karibu kila kitu. Hata matatizo, asilimia 80 ya matatizo yote yanaletwa na asilimia 20 ya mambo unayofanya au watu unaohusiana nao.

Kama tunajua kwamba kuna vichache vinaleta faida kubwa, na vingi vinavyoleta faida kidogo, kwa nini bado tunang’ang’ana na kufanya vingi? Kwa nini bado tunakazana kufanya kila kitu? Kama tuna wateja wachache ambao wanaleta faida nzuri na wengi ambao wanaleta matatizo mengi, kwa nini bado tunang’ang’ania wateja wote? Au tunawapa uzito sawa? Kama tunajua vingi tunavyofanya havizalishi, kwa nini bado tunafanya?

Kwa sehemu kubwa tunafanya kwa sababu hatujui, au tunafanya kwa sababu tunahofia kama tusipofanya vyote tutapoteza. Lakini hofu hii haitusaidii chochote, zaidi ya kutuonesha kwamba hiki ndiyo kitu muhimu kwetu kufanya.

SOMA; Punguza Nafasi Za Watu Kukuumiza Kwa Kufanya Hivi.

Leo nakushirikisha kitu kimoja muhimu cha kufanya na kitu hicho ni kupunguza nusu.

Vipi kama ukipunguza nusu ya shughuli unazofanya sasa, ukapanga kila unachofanya, na kuangalia manufaa na gharama zake, halafu ukapunguza nusu, yaani vile ambavyo havina mchango mkubwa ukaacha kabisa kuvifanya?

Vipi kama katika wateja wako wote, ukawaangalia na kuona wapi wenye faida na wapi wenye changamoto nyingi, ukapunguza wale nusu wenye changamoto na wasio na faida na kubaki na wale nusu ambao unaweza kuwahudumia vizuri?

Kwa kupunguza nusu, unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuondokana na changamoto zisizo za lazima, na pia kutoa huduma nzuri kwa nusu iliyobakia.

Fanya tathmini leo, jua ni nusu ipi unayoweza kuondokana nayo na mambo yako yakawa vizuri kabisa,

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.