Moja ya sababu kubwa zinazowazuia watu kufanikiwa, ni kukataa kuuangalia ukweli. Kwa kuwa ukweli haupo vile wanavyotaka wao, basi wanachofanya ni kutokuuangalia, bali wanaangalia kile kinachowafurahisha kwa wakati husika.
Ukweli ni kwamba maisha ni magumu, na haijalishi wewe ni nani na unaanzia wapi, kila mtu ana magumu yake kwenye maisha, kila mtu ana mlima wake anapanda na kila mtu ana vita yake anapigana. Lakini wengi hawapendi kukubali hili, badala yake wanapoteza muda kutafuta njia ya mkato ya maisha, njia rahisi ya kufanikiwa, na wanajikuta wakipoteza fedha, muda na hata maisha.
Unapoangalia ukweli, maana yake unaona kipi cha kufanya, hatua zipi za kuchukua ili uweze kupata kile unachotaka.
Pamoja na maisha kuwa magumu, lakini zipo habari njema. Vitu vingi unavyotaka kwenye maisha yako, vinawezekana, ikiwa utakuwa tayari kuuangalia ukweli, kujua unapoanzia, kuhesabu gharama unazopaswa kulipa na kuweka kazi. Kwa kuangalia hivi, utajua kipi unapaswa kufanya na kwa wakati gani, na kufanya hivyo itajiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.
SOMA; Ukweli Haulazimishwi…
Kuangalia ukweli kunatisha, hasa pale unapoanzia chini kabisa, na wanaokuzunguka wanaweza kukumaliza kabisa, kwa kukuambia huwezi au unapoteza muda. Lakini nikuhakikishie kitu kimoja, yeyote unayeona amefika juu leo, alianzia chini kabisa, na huenda chini kuliko wewe. Hivyo usikate tamaa, endelea na mapambano.
Sumu kuu itakayokupoteza ni kama utaacha kuangalia ukweli na kuingia kwenye mkumbo wa kujifurahisha na raha za muda mfupi, huku maisha yako yakizidi kuwa hovyo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK