UKURASA WA 817; Usimpe Mteja Majukumu Ambayo Siyo Yake….

By | March 27, 2017

Watu wengi wamekuwa wanafanya biashara kwa starehe sana, yaani kuna majukumu yao ambayo hawataki kuyafanya wao, bali wanataka wateja ndiyo wafanye majukumu hayo. Halafu ukiangalia majukumu hayo ni madogo sana, lakini hawayaelewi na hivyo kuwapotezea wateja.

IMG-20170316-WA0010

Siku moja nilikuwa napita mahali, nikaona pamewekwa tangazo tunauza mayai. Nikasimamisha gari na kwenda kuulizia, ni nyumbani kwa mtu na siyo eneo la biashara. Wakaniambia mayai yapo, na bei, nikatoa fedha kusubiria kuletewa mayai. Binti aliyepokea fedha akaenda kisha akarudi, akaniambia inabidi uwe na mfuko wako wa kubebea, hatutoi mifuko ya bure. Sikutaka kubishana naye, nilimwambia basi naomba unirudishie fedha yangu, akaenda ndani akarudi na mayai kwenye mfuko.

Nilitafakari tukio hili kwa dakika chache sikuelewa wazi nini kilipelekea yeye kunijibu vile awali. Nikaona labda wamezoea wateja wao wanakuja na mifuko yao, na hivyo kutokutoa huduma ya mifuko. Au labda kuweka mifuko ni gharama kubwa kwao. Lakini nilifikia muafaka kwamba, wanafanya biashara kwa mazoea, au wanataka majukumu yao yafanywe na wateja.

SOMA; Majukumu Makubwa Matano Kwa Kila Mmiliki Wa Biashara Kuzingatia.

Huu ni mfano mmoja mdogo, lakini ipo mingi zaidi.

Kwa mfano mara ngapi umeenda kununua kitu ukaambiwa hakuna chenchi, au umeenda kununua kitu asubuhi na mapema, na una fedha kubwa, halafu mtu anakushangaa, asubuhi yote hii na fedha kubwa. Sasa hapo nashindwa kuelewa, ni jukumu la mteja kuja na chenchi yake iliyokamilika?

Huo ni upande wa biashara za wengine, lakini je vipi biashara zetu binafsi?

Ni mara ngapi tumekuwa tunawategea wateja wafanye majukumu yetu binafsi? Mara ngapi tumekuwa hatujisumbui na kutaka wateja ndiyo wasumbuke? Mifano niliyotoa hapa, na vingine vingi tunavyofanya kwenye biashara, vinawafanya wateja wakipata sehemu nyingine wanayohudumiwa vizuri waachane na sisi.

Beba majukumu yako ya kibiashara, hata kama ni magumu, hakuna aliyekulazimisha kufanya hiyo biashara, ulichagua mwenyewe. Hivyo usitake wateja wakuonee huruma, kama biashara inakuwa ngumu achana nayo na fanya nyingine. Usitake wateja waone namna biashara ngumu kwako hivyo wafanye sehemu ya majukumu yako. Wakipata mwingine anayewapa huduma nzuri, watakuacha.

Kumbuka wateja hawana undugu na wewe, wala hawana ndoa na wewe ya kufa na kuzikana, muda wowote wanaweza kukucha na kwenda kwa mfanyabiashara mwingine anayewahudumia vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.