UKURASA WA 822; Badili Hadithi Unayoishi…

By | April 1, 2017

Unafanya unachofanya sasa, kutokana na hadithi ambayo umechagua kuishi. Inawezekana hadithi huyo umetengeneza mwenyewe au umeibeba kutoka kwa wengine. Mabadiliko kwa wengi yanakuwa magumu kwa sababu wanajaribu kubadili wanachofanya, au kubadili tabia kabla ya kubadili ile hadithi wanayoiishi.

IMG-20170228-WA0007

Hadithi ina nguvu kubwa sana kwetu, na inatufanya tuendelee kuwa pale ambapo tulipo, kwa sababu ndiyo tumezoea na ndiyo tunafanya.

Unafanya kazi au biashara unayofanya sasa, kwa sababu ya hadithi uliyonayo. Huenda hadithi yako ni kwamba watu kama wewe, waliosomea ulichosomea wewe hawana njia nyingine ya kukitumia zaidi ya kuajiriwa. Au hadithi inaweza kuwa kwamba biashara yako haikui, kwa sababu mazingira uliyopo ni magumu.

Huenda pia hadithi hii inakuwekea ukomo kwenye mambo mengi, kwenye hatua unazochukua, kwenye namna unavyofanya mambo yako. Vyote hivyo vinatokana na hadithi ambayo unaiishi. Hadithi hii ina nguvu kubwa mno. Kuanzia ile dhana kwamba watu wa jinsia fulani huwa hawafanyi hivyo, au kabila fulani huwa hawafanyi hicho au wanafanya hichi.

SOMA; Umuhimu Wa Hadithi Ya Biashara Yako.

Hadithi zipo na tunazitengeneza kwenye vitu mbalimbali, kwenye dini, elimu, hali ya maisha, mazingira na kila kitu cha maisha.

Ninachotaka kukuambia leo rafiki ni hichi, badili hadithi ya maisha yako. Kama kwenye hadithi yako kipo kitu chochote ambacho kinakupa ukomo, au kipo kitu ambacho kinakuzuia kuchukua hatua kubwa ili kufanikiwa, achana nacho, badili hadithi hiyo.

Jijengee hadithi inayokupa uhuru wa kuchukua hatua kubwa, jenga hadithi ambayo inakuhamasisha kuchukua hatua. Na hii itakuwa nguvu kubwa inayokusukuma ufanikiwe. Jenga hadithi ya ukweli kuhusu wewe na kuhusu mazingira yanayokuzunguka, hadithi ambayo itakuwezesha kuchukua hatua kubwa ili kufikia mafanikio makubwa sana.

Na kama ambavyo nimekuwa nakuambia rafiki, mafanikio ni maamuzi yako binafsi, kwa sababu hakuna aliyekulazimishia hadithi ulizonazo ambazo zimekufanya unase pale ulipo. Unao uwezo wa kutoka hapo, kama utabadili hadithi ya maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.