UKURASA WA 831; Ukuta Usioonekana…

By | April 10, 2017

Zamani ulikuwepo ukuta halisi, ukuta unaoonekana ambao unawazuia watu kufanya kile ambacho walitaka kufanya.

Palikuwepo na wafanyabiashara wachache sana, hivyo kuingia kwenye biashara yoyote ilikuwa ni vita, kwa sababu ungefanyiwa hujuma mpaka ukimbie mwenyewe.

Palikuwepo na studio chache za kurekodi muziki hivyo mtu akikuambia wewe huwezi kuimba ndiyo imetoka, huna tena namna.

Palikuwepo na wachapaji wachache wa vitabu, hivyo ukimpelekea kitabu chako achape, akikuambia hakifai, ni hakifai, huna njia mbadala ya kukichapa.

Lakini sasa mambo yamebadilika, kila ukuta umeanguka, hakuna tena vizuizi vikubwa ya kuwarudisha watu nyuma.

Kuna kila aina ya biashara kufanya sasa, wala hakuna atakayehangaika na wewe, maana kila mtu sasa anaingia kwenye biashara.

Kuna studio nyingi za kurekodi muziki, na kama hizo zimekushinda, unaweza hata kurekodi mwenyewe kwa simu yako ya mkononi na ukawashirikisha wengine.

Wapo wachapaji wengi wa vitabu, na hata hao wakikusumbua unaweza kuamua kuchapa wewe mwenyewe na kuwauzia wale ambao wanakihitaji.

Hakika hizi ni zama za kipekee, zama zisizokuwa na ukuta wa aina yoyote ile.

Lakini sasa cha kushangaza, bado watu hawafanyi. Pamoja na urahisi wa kuingia kwenye biashara, bado watu hawaingii kwenye biashara, pamoja na urahisi wa kurekodi, bado watu wanakufa na miziki ndani yao. Na pia pamoja na urahisi wa kuchapa, bado watu wanakufa na vitabu vizuri ndani yao.

Hapo ndipo unagundua ya kwamba, upo ukuta ambao hauonekani. Kwa nje hatuoni ukuta wowote, lakini ndani ya akili na mawazo ya mtu, amejijengea ukuta. Amejipa sababu kwa nini asianze biashara sasa, kwa sababu labda hayupo tayari au hajui ni biashara gani afanye. Hataki kurekodi japo anasukumwa kufanya hivyo kwa kujiambia hakuna atakayemsikiliza. Hataki kuandika kitabu japo kitabu kinawaka ndani yake kwa sababu anajiambia hakuna atakayesoma kitabu chake.

Ukuta usioonekana ni ukuta mbaya na mgumu sana, kwani hakuna wa kukusaidia kuuvunja ila wewe mwenyewe.

Na mimi rafiki yako nakuambia hivi, kama kuna kitu chochote kinachowaka ndani yako, tafadhali sana kifanye, anza kukifanya hata kwa hatua ndogo na usikubali kabisa kuacha. Sababu yoyote unayojipa sasa jua ni ukuta, na mara nyingi ukuta hujengwa na hofu. Kama ni biashara unayoifikiria muda mrefu anza, usisubiri maandalizi, huwa hayaishi. Kama ni kitabu unafikiria kuandika, leo hii kaa chini na andika sura kumi za kitabu hicho, na anza kukiandika mara moja.

Usikubali ukuta unaojenga mwenyewe ukutenge na mafanikio yako. Bomoa kila aina ya ukuta kwa kufanya kile ambacho unataka sana kukifanya. Utajifunza mengi sana kwa kufanya kuliko kukaa tu pembeni na kuangalia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.