Wanasema moja ya vitu vinavyofanya maisha kuwa magumu sana hapa duniani, ni kuishi na wengine vizuri. Waswahili wanasema kuishi na watu kazi, na ni kazi kweli hasa usipokuwa na maarifa sahihi ya namna ya kwenda na wengine.
Kwanza kabisa unahitaji watu, huwezi kufanikiwa bila watu, kwa sababu mafanikio yako huyaleti mwenyewe, bali watu wana mchango kwenye mafanikio yako.
Unahitaji watu wa karibu ambao wanahusika na maisha yako ya kila siku, hawa ni familia. Unahitaji pia marafiki ambao kuna mambo mnaendana, unahitaji wateja wa biashara, unahitaji watu wa kukuajiri, unahitaji watu wa kushirikiana nao kwenye biashara.
Kwa umuhimu huu wa watu, utashangaa watu hawajui namna gani waende vizuri na watu. Na hili ndiyo nataka tushirikishane siku ya leo ili kuweza kupiga hatua kwenye maisha yetu.
Kitu muhimu sana unachopaswa kuboresha ili kuweza kwenda vizuri na watu na kufanikiwa, ni mahusiano yako na wengine. Unahitaji kuboresha mahusiano yako na wale wanaokuzunguka, kuanzia nyumbani mpaka eneo lako la kazi au biashara.
SOMA; Kauli KUMI Za Confucius Zitakazokuhamashisha Kuboresha Maisha Yako.
Mahusiano yako yoyote yanapokuwa mabovu, yanatumia nguvu zako nyingi ambazo ungeweza kuzitumia kwa mafanikio yako. Utajikuta unasumbuka sana kiasi cha kuona haina maana kuendelea kuweka juhudi, kwa sababu uliotegemea wawe msaada kwako wanakuwa changamoto kwako.
Hivyo mara zote boresha mahusiano yako na wengine, usitake kuwa sahihi wakati wote, toa msaada pale unapoweza na mara zote waangalie watu kwa mchango walionao kwenye maisha yako. Hata kama watu wana mapungufu kiasi gani, angalia ni mchango gani wanao kwenye maisha yako. Kama mchango huo ni muhimu, basi boresha mahusiano yenu ili kila mmoja aweze kunufaika.
Lakini pia hii haimaanishi umvumilie kila mtu hata anayefanya maisha yako yawe magumu bila ya sababu. Ukiona wapo watu wa aina hiyo kwenye maisha yako, hata licha ya wewe kujaribu kuboresha mahusiano bado wanayaharibu, basi achana nao na songa mbele. Maisha ni mafupi sana kuyapoteza kufanya vitu ambavyo havina mchango kwenye mafanikio yako.
Mwisho kabisa usitegemee furaha yako kutoka kwa wengine, na wala usiwe mzigo kwa wengine. Watu hufanya makosa ya kufikiri wengine ndiyo watawapa furaha, na hili huwaumiza zaidi pale wanapokosa furaha hiyo. Pia wengine huwa mzigo kwa wenzao kwa sababu tu wana mahusiano mazuri, unapokuwa mzigo kwa watu, unawafanya watafute njia ya kukukimbia.
Mahusiano yako na wengine ni kiungo muhimu cha mafanikio yako, yaboreshe kila siku ili uweze kufikia mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK