Kuna watu ambao wanahitaji sana msaada, lakini jaribu kutaka kuwasaidia, watakataa kabisa kwamba hawahitaji msaada wako. Hili ni jambo la kushangaza sana, lakini ndivyo ukweli ulivyo. Kadiri mtu anahitaji kitu sana, ndivyo inavyokuwa vigumu kwake kukikubali.
Kwa mfano, mtu asiyejua, au anayefanya kitu kwa viwango vya hovyo sana, ukijaribu kumwelewesha na kumshauri njia bora zaidi ya kufanya, atakukatalia kabisa. Atakuwa mbishi sana na hatochukua ushauri wake, ataendelea kufanya yale anayofanya.
Mtu ambaye ni masikini kupindukia, unakuta ndiyo wa kwanza kukataa na kupinga pale anapopewa njia ya kuondoka kwenye umasikini aliopo. Atakuja na sababu kwa nini unachomwambia hakifai, au hakimfai yeye.
SOMA; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…
Hili liko hivyo kwa sababu watu hao ndivyo walivyo, umewakuta pale walipo kwa sababu siku zote wamekuwa wanakataa kutoka hapo walipo. Kikubwa wanachokazana kufanya, ni kuhakikisha hawatoki pale ambapo wapo.
Ninachotaka kwako rafiki ni ujiangalie kwenye kila eneo la maisha yako, je yapo maeneo ambayo unahitaji msaada kweli lakini unaukataa? Vipo vitu ambavyo hujui, lakini wanaojua wanapojaribu kukujulisha unakuwa mbishi? Huwezi kujua hili kama hutakaa chini na kujihoji bila ya hisia. Fanya zoezi hilo ili ujue maeneo yapi yanakukwamisha na uweze kuyavuka na kusonga mbele.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK