Nimekuwa nasema, maana rahisi kabisa ya utajiri na umasikini ni kwenye fedha na kazi. Pale ambapo wewe unaifanyia kazi fedha, yaani bila kufanya kazi huwezi kupata fedha ya kuendesha maisha, basi huo ni umasikini. Na pale ambapo fedha inakufanyia kazi wewe, yaani hata kama hufanyi kazi moja kwa moja bado fedha inaingia, huo ni utajiri. Najua kwa maana hii wapo wengi hawatafurahia hali zao na hivyo inabidi iwe hasira ili kuhakikisha unaondoka kwenye kundi la kuifanyia kazi fedha.
Sasa hilo siyo ninalotaka tujadili leo, bali tunachojadili ni pale watu wanapolichukulia hilo tofauti. Mfano nilikuwa nawaambia watu unahitaji kufanya kazi muda mrefu sana ili kuondoka kwenye umasikini. Kufanya kazi saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni, jumatatu mpaka ijumaa, haitoshi kukutoa kwenye umasikini. Mtu akaniuliza, sasa hapo si unakuwa unaifanyia kazi fedha? Kwa nini tusitafute njia ya fedha kutufanyia kazi? Na hapa ndipo nilipoona namna watu wanachukua hili kinyume.
SOMA; Tabia Moja Inayowaingiza Watu Wengi Kwenye Madeni Ya Kifedha, Na Namna Ya Kuiepuka.
Ipo hivi, japokuwa kila mtu lengo ni fedha imfanyie kazi, hutalala na kuamka na ghafla fedha inakufanyia kazi. Bali utaanza kuifanyia kazi, tena sana, ili kutengeneza mfumo wa yenyewe kukufanyia wewe kazi. Pale unapoanzia chini, unapoanzia kwenye umasikini, huna budi bali kuweka kazi kubwa na ya kutosha, tena kwa muda wa ziada ukilinganisha na wengine wanavyofanya. Kazi hii ndiyo itakuwezesha wewe kuitumikisha fedha baadaye.
Hivyo rafiki, elewa kwamba kabla fedha haijakufanyia kazi wewe, lazima uifanyie kazi sana. Usijidanganye unaweza kufikiri na kuja na njia ya kuweza kuitumikisha fedha kabla hujaitumikia, labda kama unataka kutumia njia ambazo siyo halali.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog