Kila mtu kuna vitu ambavyo anataka kuwa bora kwenye maisha yake na shughuli zake.
Labda unataka kuwa baba/mama bora kwa watoto wako.
Au unataka kuwa mke/mume bora kwa mwenza wako.
Huenda unataka kuwa mwajiriwa bora kwa mwajiri wako, au mwajiri bora kwa wafanyakazi wako.
Huenda unataka kuwa mfanyabiashara bora kwa wateja wako.
Pia inawezekana unataka kuwa kiongozi bora kwa wafuasi wako.
Yote hayo yanawezekana, ila hayaanzii na hapo unataka. Bali yanaanza na wewe kuwa bora kwanza, yaani unaanza kuwa mtu bora, halafu hayo mengine ndiyo yanafuata.
Hii ina maana kwamba, huwezi kuwa mfanyabiashara bora, kama hujawa kwanza mtu bora. Unaanza kuwa bora wewe kama wewe, halafu hayo mengine unayoyataka ndiyo yanafuata.
Unajua kwa nini unahitaji kuanza kuwa bora kwanza?
Kwa sababu kila unachotaka kuwa bora kwenye maisha yako;
Kinahitaji uwe na nidhamu ya hali ya juu sana.
Kinahitaji uwe na misingi ambayo unaisimamia kila siku.
Kinahitaji uwe na maono makubwa ambayo unayafanyia kazi.
Na kinahitaji ujitoe, na kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
SOMA; Maamuzi Yoyote Ni Bora…
Sasa kama wewe mwenyewe hujawa bora, kwa kujijengea yote hayo, huwezi kuwa bora kwenye kingine chochote. Ni sawa na kutaka kujenga nyumba, ila unataka uanze na paa. Ni kitu kisichowezekana kabisa.
Lakini utashangaa watu wakikazana kufanya. Hasa kwenye biashara, ambapo wengi huamini biashara ni kununua na kuuza tu, huhitaji mengine mengi. Na hapo ndipo wanapokutana na changamoto nyingi kwenye kila hatua wanayopiga, kwa sababu wanakosa yale muhimu ya kuwawezesha kuwa bora.
Unahitaji kuwa bora wewe kwanza, kabla hujataka kuwa bora kwenye jambo jingine. Kuwa bora wewe ndiyo msingi muhimu utakaoutumia kujenga chochote unachotaka kwenye maisha yako. Usikimbie msingi, kama kweli unataka kujenga kitu imara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog