Katika safari ya maisha ya mafanikio, kile unachofanya, kinahusika sana kwenye mafanikio yako. Na wengi wamekwama kufanikiwa kwa sababu kile wanachofanya kinawazuia. Kile wanachofanya, iwe ni kazi, biashara au chochote, kinakuwa kikwazo kwao kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Na sababu kuu ni kwamba wengi huona kama wanapita tu. Huwa wanaona pale walipo sasa siyo wanapotaka au wanapopaswa kuwepo, na hivyo kutokuweka mkazo unaostahili. Wanafanya kile wanachofanya, huku wakifikiria vitu vingine tofauti kabisa.
Sasa kama mawazo, akili, nguvu na mapenzi yako yote hayapo kwenye kile unachofanya, ni vigumu sana kufika mbali. Hutaweza kufanya makubwa, kwa sababu dunia haitakuacha.
Cha kushangaza, watu wamekuwa wakifanya hivi miaka na miaka, na kwa namna hii wanakuwa wameamua kupoteza sehemu kubwa ya maisha yao. Wanafanya vitu ambavyo haviwasukumi kutoka ndani yao. Badala yake inakuwa na msukumo wa nje pekee, ambao ni kupata fedha au kuonekana na wengine.
SOMA; Mabadiliko Ya Haraka Yanashindwa Haraka…
Hali hii ni mbaya kwa sababu mtu anapokaa na kuyatafakari maisha yake, anaweza kuona kama hajaishi, kitu ambacho ni kweli. Hiyo inaweza kupelekea mtu kujiona hafai na hivyo kuzidi kuwa hovyo zaidi.
Njia pekee ya kuweza kuondokana na hali hii ni kubadili kile ambacho mtu anafanya. Kama unafanya kazi au biashara ambayo haina msukumo wowote kutoka ndani yako, basi unahitaji kufanya mabadiliko, ili uweze kufanya kitu ambacho kina msukumo kutoka ndani yako.
Lakini siyo mara zote hilo linawezekana, kutokana na changamoto nyingi za maisha. Na hapo ndipo unapopaswa kufanya hili muhimu; kubadili mtazamo wako juu ya kile unachofanya. Badala ya kuangalia tu ni nini unafanya, hebu anza kuangalia watu wananufaikaje na kile unachofanya. Anza kuangalia ni msaada upi unaoutoa kwa wengine kupitia unachofanya. Maisha ya wengine yanakuwaje bora zaidi kupitia wewe.
Kwa mtazamo huu utaona ni namna gani kile unachofanya ni muhimu. Utaona fursa nyingi zaidi za kufanya mambo makubwa kwa wengine. Na utaanza kupenda kile unachofanya, utaweka juhudi kwenye kufanya na hatimaye kuweza kupata matokeo bora sana.
Kama huwezi kubadili kile unachofanya, basi anza kwa kubadili mtazamo wako juu ya kile unachofanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog