UKURASA WA 897; Hamasa Inapatikana Hapa….

By | June 15, 2017

Ili kufanikiwa, lazima tufanye mambo ambayo wengine hawapo tayari kufanya, na hata sisi wenyewe, hatujawahi kufanya hapo awali. Mambo haya siyo rahisi, na ndiyo maana wengi hawafanyi.

Hivyo kuweza kufanya mambo haya magumu na makubwa, tunahitaji sana hamasa. Lazima tuwe na hamasa ya kuweza kufanya hata pale ambapo hatuoni urahisi au matokeo mazuri.

Swali ni je hamasa tunayotaka inatoka wapi? Hapa ni muhimu kwani kumewazuia wengi kuweza kufanikiwa.

Wengi wamekuwa wanasubiri mpaka wapate hamasa ndiyo wafanye. Unajua nini kinatokea? Wanasubiri milele, maana hamasa huwa haiji yenyewe. Unaweza kusoma maisha ya wengine ambao wamefanya na ukahamasika, lakini hamasa hiyo huwa haidumu. Unaweza kuwaangalia wengine wakifanya na ukahamasika, ila utakapoanza kufanya wewe na kukutana na changamoto, hutadumu.

Hamasa bora kabisa ya kufanya mambo makubwa inatengenezwa, ndiyo, wewe mwenyewe unajitengenezea hamasa ya kuweza kufanya makubwa. Na hamasa hii inatengenezwa kwa kuanza kufanya. Siyo kusubiri, bali kuanza kufanya kile ambacho unataka kuhamasika kufanya.

SOMA; Hamasa Ni Moja Ya Kazi Zako…

Njia bora ya kutengeneza hamasa kwenye kufanya, ni kupanga kile unachotaka kufanya kwenye makundi madogo madogo. Unapofanya na kukamilisha kundi moja, unakuwa na hamasa ya kuenda kundi jingine.

Kwa mfano kama unataka kuandika kitabu ila huna hamasa, kusubiri mpaka hamasa ije itakuchukua muda. Badala yake unaweza kugawa kitabu hicho kwenye sura na kila sura kugawa vipengele kadhaa. Kisha ukajiwekea lengo la kila siku kuandika kipengele kimoja. Ukimaliza kipengele kimoja unahamasika kwenda kipengele kingine. Kwa njia hii hamasa inajengeka.

Pia unaweza kutengeneza hamasa yako kwa kuwa na picha kubwa ya kile unafanya, kuwa na maono makubwa na kuwa na kusudi kubwa la kile unachofanya. Kwa kuona namna kile unachofanya kinawasaidia wengine kunakupa hamasa ya kufanya ili wengine wapate msaada wanaopata kupitia wewe.

Ninachosema usikae ukisema ukihamasika utafanya, badala yake anza kutengeneza hamasa ambayo itakusukuma kufanya, kuanzia sasa, hapo ulipo. Jua kusudi kubwa la wewe kufanya, na anza kufanya. Hamasa itajengeka ndani yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.