Niliwahi kushuhudia ajali moja siku za nyuma sana, ambapo dereva alikuwa anamkanyaga mtu, watu wakapiga kelele sana ‘unagongaaa!’ dereva akataharuki, akarudi nyuma akamkanyaga zaidi mtu yule na kupelekea kumuumiza zaidi ya alivyofanya awali.
Hayo yote yalitokana na dereva kutaharuki, unapotaharuki kichwa kinakuwa hakijatulia na hivyo kushindwa kufanya maamuzi sahihi.
Siku za nyuma pia kulikuwa na ajali nyingi sana za moto kwenye shule za bweni, katika ajali ya aina hiyo, shule moja, wanafunzi wengi walikutwa wamefia mlangoni. Hii inaonesha walikuwa wanakazana kutoka nje, lakini kwa kuwa walikuwa wametaharuki, walitumia muda mwingi kila mmoja kutaka atoke kwanza, kilichotokea wengi wakafa pale. Huenda kama walitulia na kuamua kutoka nje mmoja mmoja, wangepona wengi zaidi.
Hata katika ajali za vyombo vya usafiri wa maji, wale wanaotaharuki ndiyo hukimbilia kurukia kwenye maji na kupoteza uhai mapema zaidi ya wengine, ambao kwa kutulia huenda wakaokolewa.
SOMA; Maamuzi Ya Kukurupuka…
Sasa hii huwa haiishii kwenye ajali pekee, hii ni tabia yetu sisi binadamu kwenye kila jambo ambalo linakwenda tofauti na tulivyotegemea, tunataharuki na kutaka kuchukua hatua ya haraka kuepusha madhara. Sasa kwa hatua hiyo tunayochukua tukiwa tumetaharuki, ndiyo tunaongeza madhara mara dufu.
Kichwa kilichotulia kinafanya maamuzi bora kuliko kichwa kilichotaharuki. Hivyo popote pale unapokuwa, na lolote linapotokea, hata kama ni kubwa kiasi gani, usikimbilie kuchukua hatua, bali tuliza kichwa na fikiri kwa makini, hatua ipi bora ya kuchukua.
Najua kwa hali ya ubinadamu unaweza kuona kufikiri ni kupoteza muda, lakini kumbuka hili, hatua yoyote ya haraka utakayochukua, kwa asilimia kubwa inakuwa na madhara makubwa mno kuliko kutokuchukua hatua kabisa. Hivyo kuchukua muda mchache na kufikiri kwa kina kabla hujachukua hatua, mara nyingi itakupelekea wewe kuchukua hatua bora zaidi.
Mara zote kumbuka, kichwa kilichotulia, kinafanya maamuzi bora. Mara zote tuliza kichwa chako kabla hujafanya maamuzi muhimu kwenye jambo lolote kubwa kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog