Watu wengi wamekuwa wanasema kwamba zama hizi tunazoishi, watu wanazama kwenye taarifa, ila hawana maarifa. Yaani pamoja na fursa nyingi sana za kupata taarifa, bado watu wanashindwa kupata maarifa sahihi kwao.
Pamoja na wingi wa vitabu vilivyoandikwa kwenye kila eneo, wingi wa magazeti, majarida na hata blogu zinazotoa mafunzo mazuri kwenye kila eneo la maisha yetu, bado watu wanakosa maarifa yanayoweza kuwasaidia.
Inasemekana kwamba, taarifa zinazozalishwa ndani ya siku moja kwa zama hizi, ni zaidi ya taarifa ambazo zilikuwa zinazalishwa kwa miaka kumi, kwenye milenia ya pili. Yaani kwa siku moja unapata taarifa nyingi, kuliko taarifa ambazo mtu aliweza kuzipata kwa maisha yake yote miaka elfu moja iliyopita.
Tatizo ni nini hapa? Kwa nini taarifa zipo lakini hatuna maarifa?
Jibu ni moja, hatujui kuuliza maswali mazuri.
SOMA; Maswali Matatu Muhimu Kujiuliza Kabla Ya Kuchukua “RISK”…
Pamoja na upatikanaji huu wa taarifa, ili kuweza kuzipata zinazotuhusu kweli na zinazoweza kutusaidia, basi tunahitaji kuuliza maswali mazuri. Dunia ina majibu yote unayotaka, swala ni je unauliza maswali gani?
Kama unauliza maswali mazuri, maswali yanayoendana na kile unachotaka, basi dunia itakupa majibu mazuri, ambayo yatakuwa maarifa sahihi kwako kuweza kufanyia kazi.
Hivyo rafiki, usiwe kama wengi ambao wanaendelea kuzama kwenye maarifa, au wanakufa kwa kiu cha ujinga kwenye bahari ya taarifa. Jifunze kuuliza maswali mazuri, yatakayokupatia maarifa ya kile unachotaka na utaweza kutumia kila taarifa inayopatikana kuwa maarifa bora kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog