Umeshawahi kukutana na kitu kipya, labda maarifa au taarifa ambazo hukuzipata mapema na kusema laiti ungejua mapema ungekuwa mbali? Umeshawahi kuona kama umechelewa sana kuchukua hatua na hivyo kuona huna la kufanya? Umekuwa unajidanganya sana kwenye hilo la kuchelewa.
Upo usemi wa wachina kwamba; muda bora wa kupanda mti ulikuwa miaka 20 iliyopita, muda mwingine bora ni leo.
Usemi huu unatuonesha ni kwa namna gani hakuna kuchelewa. Chochote ambacho tulikuwa hatujui na tumejua sasa, jukumu letu kuu ni moja, kuchukua hatua sasa. Kadiri tunavyochukua hatua pale tunapojua kile ambacho tulikuwa hatujui, ndivyo tunavyonufaika na kile ambacho tumekijua.
Tatizo la watu wengi ni kupata hamasa pale wanapojua kitu kipya, halafu hawachukui hatua kunufaika na kile walichojua. Hapo sasa mtu anakuwa amechagua yeye mwenyewe kuchelewa.
SOMA; Jukumu Muhimu Kwenye Maisha Yako Ambalo Huenda Bado Hujalifanya.
Kujua kitu ambacho unapaswa kufanya, halafu hufanyi, kunakuumiza wewe unayejua kuliko yule ambaye hafanyi kwa sababu hajui. Hivyo ukishajua, usijilinganishe na wengine ambao hawajui, kwa kutofanya kwa sababu na wao hawafanyi.
Njia nyingine ya kutumia dhana hii ya hakuna kuchelewa ni kuepuka kutapeliwa. Mara nyingi matapeli hutumia hofu ya kukosa kuwasukuma watu kuchukua hatua. Wanakuambia utakosa fursa hii ya kipekee ambayo huwezi kuipata tena. Kwa kujua kwamba hakuna kuchelewa, utafanya mambo yako kwa umakini na huwezi kutapeliwa. Fursa huwa haziishi, ukiikosa moja jua kuna nyingine nyingi zinakuja, ni wewe tu kujua unataka nini na kuweza kuchukua hatua.
Ukishajua ambacho ulikuwa hujui, kitumie kupiga hatua. Kuchelewa ni pale unapojua nini unapaswa kufanya, halafu unaamua kutokufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog