Dunia tayari ina waongeaji wa kutosha, wale ambao wanajua nini kinapaswa kufanya, wanaosema watafanya, lakini haifiki hatua wakakaa chini na kufanya au wakaonesha mfano namna gani ya kufanya.
Hivyo dunia kwa sasa, haihitaji tena mwongeaji mwingine, badala yake inahitaji watu wa kufanya kitu, hata kama ni kitu kidogo kiasi gani.
Dunia haihitaji watu wanaosema siku moja wataingia kwenye biashara, bali inataka watu wanaosimama na kuanza biashara zao, hata kama hawana pakubwa pa kuanzia.
Dunia haihitaji watu wanaolalamika namna mambo yanavyoenda, bali inahitaji watu wanaofanya kitu, kubadili yale ambayo hawayataki.
Na usifikiri dunia inataka ufanye makubwa sana, inataka ufanye madogo madogo tu, ila uyafanye kweli, siyo kwa kujaribu.
SOMA; Dhibiti Dunia Yako…
Na mambo yenyewe madogo madogo ni kama kuwa mwema, kuongeza thamani kwa wengine, kusimamia unachoamini, kurekebisha ambapo hapajakaa sawa.
Usipoteze muda wako kujaribu kuipigia dunia kelele, haitakusikia, kwa sababu tayari kelele zipo nyingi sana.
Kitu pekee unachoweza kufanya na dunia ikakuona, ni kuchukua hatua, kubadili kitu, kuongeza thamani, chochote unachoweza kufanya na kikaleta tofauti, dunia itaona na itakukubali kwa hilo.
Kusema nini kinapaswa kufanywa, au nini unapanga kufanya, ni kujipotezea muda wako mwenyewe. Fanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog