Japokuwa watu wanapenda kusema usihukumu kitabu kwa ganda la nje, lakini kila mtu ndiyo kitu anachofanya, katika maamuzi yake mengi kwenye maisha. Pale ambapo hatujui kitu, au hatuna uhakika nacho, basi tunatumia zaidi mwonekano wake wa nje katika kufanya maamuzi.
Ni rahisi kusema huna haja ya kufanyia kazi mwonekano wa nje kwa sababu ndani pako vizuri, lakini kabla watu hawajaamua kuangalia ndani, wanavutiwa au kufukuzwa na mwonekano wa nje.
Hivyo kuwa bora sana ndani, namaanisha kuanzia mambo yako binafsi, kazi zako na hata biashara. Lakini pia kuwa bora sana kwa nje, kuanzia mwonekano wako, ufanyaji wako kazi na mengine yote yanayoonekana kwa nje.
Na hapa siyo kwamba unataka kujionesha, ila unawapa watu sababu ya kuanza na wewe, kabla hawajafikiria pengine popote. Mwonekano wa nje ukiwa mzuri unawapa watu imani kwamba ndani pia patakuwa pazuri. Lakini mwonekano wa nje ukiwa mbaya, unawapa watu wasiwasi kwamba huenda ndani mambo yakawa mabaya zaidi.
SOMA;Binadamu Ni Viumbe Wa Kuhukumu, Hivi Ndivyo Unaweza Kuepuka Madhara Ya Hukumu Zao.
Na mwisho kabisa, kama huwezi kujali nje ambapo watu wanaona, je utaweza kujali ndani?
Nje kwa maisha yako binafsi ni mavazi yako, unadhifu wako, ongea yako, tabia zako za kimwili. Ndani kwenye maisha yako binafsi ni mawazo yako, ujuzi wako, uzoefu wako na mtazamo wako.
Kadhalika kwenye kazi na biashara, nje ni kile ambacho mtu anaona kwanza kabla hajafanya maamuzi ya kujihusisha na wewe, na ndani ni kile anachopata kwa kujihusisha na wewe. Kuwa makini na ndani, lakini hakikisha nje pako vizuri pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
asante sana kwa darasa zuri kwa maboresho maisha yetu.
Karibu.