Tofauti ya wale wanaoweza kufanya makubwa licha ya kuwa na changamoto na wale wanaokata tamaa na kuacha, siyo ukubwa wa changamoto, wala siyo uwezo wa kifedha au kiakili, bali ni tofauti ya mtazamo.
Wale wanaokata tamaa na kuacha ni wale ambao wakikutana na changamoto wanajiambia hakuna ninachoweza kufanya. Nimejaribu sana lakini imeshindikana. Hakuna tena namna, inabidi nifanye kitu kingine. Safari inaishia hapo na hakuna kikubwa wanaweza kufanya.
Lakini wale wanaofanya makubwa, wale wanaovuka changamoto na kupata matokeo makubwa, wanapokutana na ugumu wanajiambia kuna njia ya kupita hapa, kuna kitu wanaweza kufanya. Na licha ya kujaribu na kushindwa, ule mtazamo wa kwamba kuna kinachoweza kufanyika huwa hautoki ndani yao. Na kweli inafika hatua wanaona kitu cha kufanya, au wanajaribu njia fulani na ndiyo inayoleta majibu.
SOMA; Usikimbilie Kufanya Vitu Rahisi, Vitakupoteza Kibiashara…
Sasa turudi kwako rafiki, unapokutana na hali yoyote ngumu au ya changamoto, kipi unachoanza kufikiria haraka? Unafikiria kwamba ndiyo mwisho na haiwezekani tena? Au unafikiria ipo njia ya kuweza kufanya, kipo kitu cha kufanya?
Anza sasa kufikiria kwamba ipo njia, hata pale wengine wote wanaposema hakuna njia, wewe sema ipo njia. Hata kama huna uhakika kwamba njia inatoka wapi, wewe amini ipo njia, na endelea kuweka juhudi kuhakikisha unaifikia njia hiyo.
Kwa mtazamo huu, mara zote utapata njia ya kutatua lolote unalokutana nalo. Na hata kama hutalitatua kabisa, angalau utapata njia mbadala ya kufika au kupata kile unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog